Kushinda Majaribu

Majaribu au Jaribu ni hali ya kushawishika kufanya mambo / jambo lisilompendeza Mungu kwa kuahidiwa / kutazamia faida fulani ya muda mfupi.
Yakobo 1:14-15 Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.
Mtu anapojaribiwa hadi kufikia kutenda dhambi anapitia hatua tatu zifuatazo:
Hatua ya Kwanza: Udadisi
Tamaa ya dhambi inamfanya mtu awe mdadisi kuhusu jambo fulani ambalo ni dhambi. Udadisi huo unamuweka katika mazingira ambayo ni ya hatari na yenye ushawishi mkubwa wa kufanya dhambi. Mtu hawezi kuungua hadi pale anapokuwa ameukaribia moto, hatua hii ya udadisi inamsogeza mtu karibu na moto huku ikimfanya ajione kama hawezi kuungua. Mfano ni jinsi ambavyo Hawa alipokuwa anaongea na shetani kuhusu mti wa ujuzi wa mema na mabaya, shetani alimdanganya kuwa akila atafanana na Mungu na kwa sababu ya udadisi wake akaingia kwenye mtego na kuanguka. Pia Daudi alivyomuona mwanamke akioga kwa mbali, akadadisi kujua ni nani na baadaye akashawishika kutenda dhambi maana hakujizuia kudadisi pale alipoona kuwa sio jambo jema.
Hatua ya Pili: Kuvutika / Kuvutwa
Wakati mtu anaendelea kudadisi anavutika na ahadi kuwa kufanya jambo hilo ambalo limekatazwa atapata faida nzuri na kufurahia. Jambo ambalo halioni katika muda huu ni kuwa faida hizo ni za muda mfupi na kamwe haziwezi kumridhisha na kumfanikisha. Hawa alidanganywa atafanana na Mungu naye akavutika.
Waebrania 11:25 akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo;
Katika hatua hii hautauona ubaya wa dhambi maana majaribu huja ili kukudanganya na kukupoteza na sio kukuonyesha ukweli na uhalisia.
Hatua ya Tatu: Kukamatwa / Kuanguka
Hapa mtu anajikuta ameshaingia kwenye jaribu kwa sababu aliruhusu kuvutwa na kudanganywa na shetani. Daudi aliingika katika jaribu na kukamatwa kwa sababu alikubali kupitia hatua zote bila kuzigundua hila za shetani. 2 Samweli 11:1-5
Ili ushinde majaribu, yakupasa…
Hapa tuangalie mfano wa Yusufu alivyofanya baada ya kujaribiwa na mke wa potifa, mwanzo 39.
1. Usikaribie wala kusogelea
Mithali 6: 27-28 Je! mtu anaweza kuutia moto kifuani pake, na nguo zake zisiteketezwe? Je! mtu anaweza kukanyaga makaa ya moto, na nyayo zake zisiungue?
Yusufu hakukubali kumsogelea mke wa Potifa maana alijua atakuwa anausogelea moto. Kujaribiwa sio dhambi, bali dhambi huja pale unaposhindwa na kuanguka kwenye jaribu.
2. Tambua kuwa hata kama dhambi inaonekana ya kupendeza ni kwa kitambo tu.
Tambua ya kuwa ni hakika ya kuwa dhambi itakupeleka kwenye maangamizo. Itakupelekea kujuta, kuhukumiwa, na kutengwa mbali na Mungu. Yusufu alijua kuwa furaha ya dhambi ya muda mfupi haitalingana na taabu itakayofuata baada yake. Hakuwa tayari kumkosea Mungu wake kwa namna yoyote ile wala kwa sababu yoyote ile.
3. Ione dhambi kama ilivyo
Mwanzo 39:9b Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?
Lazima uitambue dhambi kama ilivyo na kufahamu kuwa ni chukizo mbele za Mungu. Ione dhambi kama Mungu anavyoiona, kwamba ni kitu kibaya kisichofaa kutendwa na mtu anayemfuata Mungu. Dhambi huwa na tabia ya kudanganya na kuja kama kitu cha kupendeza, Yusufu hakukubali kudanganywa. Usifanye dhambi kwa kujidanganya sio kosa kwa sababu kila mtu anafanya hivyo au utafanya mara moja tu, dhambi ni dhambi!
Mungu akubariki unaposhindana na majaribu na kuyashinda kama Yusufu.

Comments

Popular Posts