Kushindana na Shetani
Maana ya jina Shetani ni
adui, au mpinzani. Baalam alipopingwa na malaika (Hesabu 22:22),
malaika yule alifanya kazi kama Shetani (ingawa hakuwa Shetani, ila
kupinga huku ni kama afanyavyo Shetani). Shetani ni adui
anayepinga. Anapinga Uungu usionekane. Maahali popote palipo pema
atapapinga na kuleta ubaya. Palipo na nuru atapinga na kuleta giza.
Palipo na kweli atapinga nakuleta uongo, palipo na uzima atapinga na
kuleta mauti. Maandiko yanasema Mungu alimwondokeshea Sulemani adui
mwingine aitwaye Rezoni (1 Wafalme 11:23). Adui huyu alimpinga
Sulemani, kama Shetani afanyavyo. Roho ya mpinga Kristo (1Yohana 4:3),
ni roho ya Shetani, inapingana na Mungu na uungu duniani (2
Wathesalonike 2:3-4).
Yesu alishamshinda
Shetani kwaajili yetu (1Wakorintho 15:57). Amemshinda na ametupa
kushinda kwake. Kumshinda Shetani huku ni kushinda ushetani, yaani
upingamizi wake. Hata hivyo Adui amebaki na kitu kimoja kinaitwa HILA.
Kwa Kiyunani hila ni methodaeias, tafsiri yake ni mbinu za kulaghai na kutega mitego. Silaha tunazivaa ili kupinga hila na sio nguvu za Shetani,
Shetani nguvu hana kwa njia ya Yesu. Yesu alimharibu kabisa msalabani!
Hatupigani naye, Yesu alishapigana naye akamshinda. Sasa tunashindania
ushindi wake, tunahakikisha unasimama wakati wote, hatuutafuti tunao,
tunashindana usimame wakati wote.
YESU AMESHASHINDA TUNAUSHINDANIA USHINDI WAKE
1.Kutii na Kupinga : Yakobo 4:7-8, 1Petro 5:7-9
Wakati
wote kaa chini ya mamlaka ya Yesu. Tenda asemayo, ishi kwa upendo, Kwa
kufanya hivi mamlaka yake itadhihirika kwako ukimpinga Shetani,
atakimbia. Ukipinga upingamizi wake atakimbia.
2.Kufahamu uwanja wa Mapambano: 2Wakorintho 11:3, 2Wakorintho 10:3-4
Kanuni
moja ya vita ni kujua adui anapigania wapi. Shetani hupingana nasi kwa
kupitia mawazo na fikra zetu. Hulenga mfumo wa mawazo. Ukiweza kumshinda
katika mawazo yako hataweza kukupata. Akikupata mawazo yako amekupata
maisha yako. Mpinge katika mawazo kwa kusema kitu kwa kinywa, si kwa
kuwaza neno tu, bali kwa kulisema. Usemapo neno kinywani linashinda mawazoni.
3.Kufahamu Silaha Yako: Waefeso 6:17
Maandiko
yameonyesha silaha kadhaa, silaha zote zinamsingi wa Neno la Mungu.
Kama vile meli inavyotegemea nanga, wakati wa mawimbi, Neno lisiache
kutoka kinywani mwako, wakati wa misukosuko tu, linashinda tu. Luka 4:1
-11, inaonyesha Yesu alidumu kusema Neno la Mungu, Shetani alipokuwa
akimjaribu au kumpinga. Alidumu na Neno kinywani mpaka Ibilisi
akamwacha, kisha malaika wakamuudumia. Udumupo kusema neno mpinzani atakuacha mbinguni watakuudumia.
4. Walio Upande Wako: Warumi 8:31, Zaburi 118:7
Katika
mawazo yako mwone Mungu yuko upande wako, Shetani anayekuchukia
ameshindwa (Zaburi 118:7). Malaika walio upande wako ni wengi kuliko
mashetani. Kanisa la Yesu au waliookoka wako upande wako, wana mamlaka
kubwa kuliko Shetani. Yesu aliye ndani yako ni mkuu kuliko Shetani!
5. Kufahamu Nafasi Yako: Waefeso 2:5-6
Yesu
yupo juu ya kila kitu (Waefeso 1:19-23), Upo juu ya kila kitu pamoja
naye (Waefeso 2:5-6). Mashetani wote na hila zao zipo chini ya kinywa
chako, Yaani neno usemalo.
6. Kukaa katika Roho: Waefeso 6:18, Yohana 4:23
Unamshinda
Shetani kwa kukaa katika Roho Mtakatifu. Unapokaa katika ufunuo wa Roho
katika kulijua neno, Unapodumu kuomba kwa Roho Mtakatifu, Unapoishi kwa
tunda la Roho na si matendo ya mwili. Unapomwabudu Mungu kwa nguvu za
Roho Mtakatifu. Wakati wote unapokuwa na ushirika na Roho kwa kuongea
naye, ni wakati kwa kumshinda adui.
7. Kukaa katika Agano: Yohana 10:28, Yohana 6:37
Shetani
hawezi kukutoa katika agano lako na Mungu kwa njia ya Yesu. Upo
mikononi mwa Yesu hakuna awezaye kukutoa hata kwa hila, mtazame Yesu
aliye ndani yako na kushinda.
Kumshinda Shetani ni Kushinda Woga
“Kwa
kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya
kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia Aba, yaani Baba”
(Warumi 8:15)
Zamani,
nyakati za biblia watumwa hawakuruhusiwa kuwaita bwana zao “Aba” yaani
baba mpendwa. Watumwa waliokuwa chini ya mwanamke hawakuruhusiwa kumwita
“Imma”. Watumwa na bwana zao walihusiana kwa misingi ya hofu. Watoto
hawakuwa na hofu waliwaita baba zao “Aba” na mama zao “Imma”, kwa
watumwa haikuwa hivyo.
Nguvu ya Shetani
Roho ya kitumwa ni roho ya dhambi, “…Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.” (Yohana 8:34). Roho hii ni chanzo cha woga, au hofu. Adamu alipotenda dhambi tu, alisema yafuyatayo mbele za Mungu, “…Nilisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi…”
(Mwanzo 3:10). Adamu alipotenda dhambi alikufa, alitengwa na Mungu,
hakufa tu! Bali pia alikuwa mtumwa kwasababu ya roho ya woga,
iliyoambatana na dhambi. Akaanza kumkimbia Mungu! Mwanzoni alimwona
kama Aba, sasa akaanza kumwogopa kama mtumwa! Wanadamu wote tukageuka
kuwa watumwa wa ibilisi kutokana na dhambi ya Adamu, Shetani akatutawala
kwa woga wa mauti, tukawa watumwa.
Yesu Ameondoa Woga
Woga
uliingia duniani kwa njia ya Adamu aliyekuwa katika mwili. Woga
unaondoka katika maisha yako kwa Yesu aliyekuja katika mwili. Yesu
amemharibu Shetani aliyetutawala kwa woga wa mauti, Akatuacha huru
(Waebrania 2:14). Katika Yesu Mungu amekuwa Baba yetu, tunamwita Aba kwa
kuwa si watumwa tena wa Shetani na dhambi kwa njia ya Yesu.
WOGA
NI MLANGO WA SHETANI KUMWINGIA MTU NA KUMTAWALA. IKIWA UMEMPA YESU
MAISHA YAKO, YESU AMEUFUNGA MLANGO HUO. UKIMTAZAMA YEYE NA KUMTAMKA YEYE
KATIKA MAZINGIRA YA WOGA YANAYOKUZUNGUKA SHETANI HATAPATA NAFASI.
Vyanzo vya Woga
1. Kuogopa Mambo Yajayo: Kwa
mfano utaishije na uchumi unazidi kuwa mbaya. Unaweza kupata mawazo
yanayoongea na kukuuliza utaishije, bila shaka itakuwa ni Shetani
anapandikiza woga ndani yako, ili kutafuta mlango katika maisha
yako. Dawa ya woga huu ni kujua Yesu ni wa kwanza na wa mwisho, yupo
sasa, amekuokoa na ameshashika na maisha yako yajayo! (Ufunuo 1:18).
2. Kuogopa Kifo: Maandiko
yanasema uhai wetu umefichwa katika Kristo. Shetani hawezi kuupata uhai
wako, labda akaunyang’anye kwa Yesu. Hauishi kwa nafsi yako unaishi kwa
njia ya Yesu, sema na kuwaza hivyo, woga wa kifo utakimbia. Woga huu ni
woga wa hatari, wenyewe ni kifo! Ukiona unaogopa kifo shindana haraka
kama unashindana na Shetani. Kwa kutamka uhai wako ndani ya Yesu
(Wakolosai 2:1-3).
3. Kuogopa Kushindwa:
Kuogopa kushindwa ni kama vile, kuogopa kuomba kazi kwa kuwa hutaiweza,
kuogopa mtihani kwa kuwa hutafaulu nk. Kuogopa kushindwa ni kujiandaa
kushindwa.
4. Kuogopa Watu: Woga mwingine mbaya ni kuogopa watu. Kila utakacho kufanya unafikiria watu kwanza, woga wa namna hii ni mtego, “Kuwaogopa wanadamu huleta mtego bali amtumainiye Bwana atakuwa salama.” (Mithali 29:25). Woga huu ujapo tamka tumaini lako kwa Mungu zaidi ya watu, utatoka katika mtego wa Shetani.
5. Kuogopa Yasiyojulikana: Mara
nyingine unaweza kujikuta unaogopa kitu kisichojulikana; Au unaogopa
kila kitu; Unaogopa watu, ukipanda basi unaogopa kiti cha basi kukalia;
unaogopa matairi ya basi yatapasuka! itabidi uongee na woga huo kama
roho. Kama kiumbe cha kishetani; kama pepo. Uiamuru itoke kwa jina la
Yesu, katika nafsi yako, pia uambie roho hiyo, hujapewa roho ya woga
(2Timoteo 1:7).
Badilisha
mfumo wako wa kufikiri, utabadilisha mfumo wako wa mitazamo, baada ya
hapo utajijengea ngome ya kutoogopa na kuangusha ngome ya woga. Ngome ya
woga ni ngome ya kushindwa, kutoogopa kwa njia ya Yesu ni kushinda.
Wakati wote jenga ngome ya kutoogopa kwa kusema maneno haya:
Isaya 51:12
Zaburi 118:6
Waebrania 13:5-6
Mathayo 10:28
Mithali 1:33
2Timoteo 1:7
Ufunuo 1:18
UPINGAPO WOGA UNAMPINGA SHETANI
Mungu na akubariki wewe na familia yako na damu ya Yesu ikutetee na kukushindia kwa hali zote unazo pitia.
wako mtumishi Mecky leo.
Comments
Post a Comment