HATUA ZA KUUKULIA WOKOVU NA NEEMA YA MUNGU KTK MAISHA YAKO.
Tangu kutungwa kwa
mimba hadi mtoto anapozaliwa, kuna hatua mbali mbali za ukuaji na majina ya
hatua hizo hutofautiana kutoka hatua moja hadi hatua nyingine. Inapotokea mtoto
amezaliwa, lakini haongezeki kimo, uzito, ufahamu licha ya kuongezeka kwa idadi
ya miaka, hicho ni kiashilia tosha kuwa mtoto huyo ana matatizo ya ukuaji
kiafya. Ni lazima wazazi wa mtoto huyo watafute msaada wa kitabibu haraka sana
iwezekanavyo.
Katika ulimwengu wa
kiroho pia, mtu yoyote anapompokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha
yake, anakuwa amepokea wokovu. Wokovu unalingana na ukuaji wa mwanadamu, ni
lazima mtu huyu aukulie wokovu na neema ya Mungu kutoka hatua ya kwanza kabisa
hadi kufikia hatua ya mwisho ambayo ni ufufuo wa uzima wa milele.
Katika somo letu hili
lenye kichwa, “hatua za kuukulia wokovu na neema ya Mungu”, tutajifunza hatua
kuu tatu ambazo mtu aliyeokoka ni lazima azipitie. Ni maombi yangu kwamba, Roho
Mtakatifu akufundishe kwa utulivu na undani ili upate kuelewa na kujitambua uko
hatua ipi na unatakiwa kwenda hatua ipi, na ufanye nini ili kuifikia hatua
iliyopo mbele yako.
Hatua za kuukulia
wokovu na neema ya Mungu, nimezigawa katika hatua kuu tatu ambazo zina hatua
nyingine ndogo ndogo ndani yake kulingana na vile Roho Mtakatifu alivyonijalia;
Kuamini na kuokoka
Kumjua Mungu,
kumjulisha Mungu kwa wengine na Mungu kukujua wewe
Kufanyika rafiki wa
Mungu
1.
KUAMINI NA KUOKOKA
(a). kuamini
Marko 16:16, aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini atahukumiwa
Yohana 3:16, kwa maana
jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu (mwanadamu), hata akamtoa Mwanawe pekee,
ili kila mtu amwaminiye asipotee,
bali awe na uzima wa milele (wokovu)
Katika mistari miwili
hiyo hapo juu, kuna kitu tunajifunza. Kitu hicho ni lazima kuamini ndipo wokovu upatikane. Kwa sababu hiyo huwezi
kupata wokovu pasipokumuamini Mungu na Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa
maisha yako.
Siyo kila mtu anayemjua
Mungu na Yesu Kristo, anamuamini Mungu na Yesu Kristo. Na siyo kila
anayemuamini Mungu anamuamini na Yesu Kristo. Na ndiyo sababu siyo wanadamu
wote tunaolisikia neno la Mungu tumeokoka.
Kwa sababu hiyo, ni
lazima mtu aamini kuwa Mungu yupo, anaishi milele, Yesu Kristo ni mwana wa
Mungu (Mathayo 16:16, Luka 1:35), aliyekufa msalabani na kufufuka ili atuokoe
(Mathayo 26:28).
Na siyo kuamini tu
Mungu yupo, ni lazima ijulikane kuwa Mungu unayemuamini ni Yehova (ndilo Jina
lake), tena anaishi milele. Ninasema hivi kwa sababu, hata wanaoabudu sanamu,
wanyama au miti mikubwa nao pia wana Imani kuwa hivyo vitu wanavyoviabudu ndiyo
miungu yao.
(b). kuokoka
Kuokoka ni kuamini kuwa
Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako, kukiri kwa kinywa imani hiyo na
kubadilika kutoka kuishi maisha ya dhambi na kuishi maisha matakatifu ya
kupendeza Mungu.
Kwa maana hiyo, imani
peke yake haitoshi kumpa mtu wokovu, ni lazima aikiri imani hiyo kwa maneno ya
kinywa chake pasipo kulazimishwa au kushawishiwa (Warumi 10:9)
Haitakiwi mtu apate
wokovu kwa kulazimishwa au kushawishiwa; kwa mfano mtu anaamua kuokoka ili amuoe
au aolewe na mtu fulani aliyeokoka. Wengi wa watu wa aina hii hawawezi kuukulia
wokovu kwa viwango vinavyostahili, kwa sababu hawakuokoka ili kumpokea Yesu
Kristo bali waliokoka ili wampate mtu fulani. Wengi wao wanakuwa na wokovu wa
kifafa.
(c). Hatua za kuokoka
(i). kuisikia injili ya
Yesu Kristo
Ni lazima uisikie
injili ya Yesu Kristo kwanza ili upate kumjua Mungu na Yesu Kristo kisha ujenge
Imani itakayo kupelekea kuupata wokovu (1 Petro 1:23, Marko 16:15-16).
(ii). Kuamini
Baada ya kuisikia injili,
kinachofuata ni kujenga imani ya ile injili uliyoisikia (Wagalatia 3:26). Na
hapa ndipo penye tatizo, kama umeisikia imani potofu basi utakuwa ukiamini na
kuabudu watu, vitu, wanyama; vitu visivyo Mungu wa kweli aliye hai.
Kwa sababu hiyo, kabla
ya kuamini ni vema ukachunguza ni Mungu yupi anayehubiriwa hapo, siyo kila
mungu anayehubiriwa anastahili kuabudiwa. Ni Mungu mmoja tu ndiye anayestahili
kuabudiwa, jina lake Yehova ambaye kupitia Yesu Kristo tunapata wokovu na uzima
wa milele.
(iii). Kuokoka
Baada ya kuisikia
injili ya Yesu Kristo, unapata Imani ya injili uliyoisikia, hatua inayofuata ni
kuokoka kwa kuikiri imani uliyoisikia na kufanyika mwanafunzi wa Yesu Kristo
ukiacha njia zote ovu na kufuata njia ya haki kama lisemavyo neno la Mungu
(Warumi 10:10).
(d). Imani ni lazima
ikue au iongezeke
Baada ya kuamini na
kupokea wokovu, hutakiwi kubaki pale pale kama jinsi siku ya kwanza ulipoamini
na kuokoka ulivyokuwa. Unatakiwa kuilinda imani na wokovu wako, na imani yako
ni lazima ikue au iongezeke, kutoka kiwango hadi kiwango, kutoka chini kupanda
juu (2 Korintho 10:15 na 2 Thesalonike 1:3).
Mpendwa msomaji wangu
ni imani yangu kuwa kuna kitu kipya Roho Mtakatifu amekufundisha, usikose
sehemu ya pili ya somo hili. Mungu akubariki sana, na akubariki zaidi kwa
kushiriki na wengine masomo haya. Amina.
Comments
Post a Comment