NAMNA UNAVYOPITA KATIKA JARIBU NDIYO KUNAAMUA NAMNA YA USHINDI WAKO

Maana na makusudi ya kujaribiwa
 Jaribu linasemekana kuwa ni mtaji wa kuinua imani ya mtu anayejaribiwa, lakini binafsi ninapenda kuirekebisha sentensi hii. Jaribu ni mtaji wa kuinua imani ya anayeshinda jaribu; kama umejaribiwa na jaribu likakuangusha, siyo sahihi kusema jaribu hilo lililokuangusha lilikuwa mtaji wa kuinua imani yako. Imani ipi? Kama umeshindwa kuitetea imani yako na kuangushwa, jaribu halikuwa mtaji kwako. 
Jaribu huja na makusudi mawili; moja, ni kumuimarisha kiroho na kuinua imani ya anayejaribiwa na kushinda jaribu. Pili, ni kumuangusha mtakatifu na kuharibu uhusiano wake na Mungu. Na mara nyingine jaribu au teso huwa ni kiboko cha Mungu cha kulirudi kanisa lake. Ninaposema kanisa ninamaanisha Mkristo.
Kuinua imani ya Mkristo. Nikupe mfano kwanza, kuna hekima ya Kimungu na hekima ya kibinadamu.  Hekima ya Kimungu hupewa mtu yoyote pasipo kujari umri, na hii huletwa na Yesu Kristo mwenyewe. Na hekima ya kibinadamu huja kutokana na uzoefu wa muda mrefu alionao mtu katika jambo fulani, na hekima hii wanayo wazee. Na imani ndivyo ilivyo, ili ikue ni lazima ipitishwe katika kujaribiwa, ipitishwe katika vitu ambavyo sayansi na akili ya kibinadamu haviwezekani. Ukiisha pita hapo kwa msaada wa Mungu kwa jina la Yesu Kristo ndipo imani yako inapokuwa. Ndipo unapozidisha imani na uhusiano wako na Mungu kupitia Yesu Kristo (Yohana 11:3-4, 14-15 na 1 Petro 1:6-7)
Kumuangusha mtakatifu. Hili ni jaribu linalosababishwa na shetani moja kwa moja, na makusudi yake huwa ni kumuangusha mtakatifu ili kuharibu na kufuta kabisa uhusiano wake na Mungu. Kwa mfano, Ayubu hakujaribiwa ili kuinua imani yake au kurudiwa na Mungu, alijaribiwa ili amkufuru Mungu, kwa Kiswahili chepesi ni ili avunje uhusiano wake na Mungu. Kwa hiyo kuna wakati shetani huwajaribu Wakristo ili awafarakanishe na Mungu (Yohana 2:10, Ayubu 2:4-5)
Kurudiwa na Mungu. Hapa naomba nieleweke, hili kwa upande mmoja siyo jaribu na kwa upande mwingine ni jaribu. Nina maana gani; kwa upande wa Mungu ni kiboko cha kulirudi kanisa lake kama ilivyo kwa mzazi anapomuadhibu mtoto aliyekosea. Kwa upande wa Mkristo, analiona kama jaribu. Na hili hutupata ikiwa tumekengeuka na kuiacha njia ya haki, tumemkosea Mungu. Na tukitubu na kuirudia njia ya haki, utaona mateso yote yanaondoka pia (Mithali 3:11-12, Ayubu 5:17)
Nini cha kufanya uwapo katika jaribu
Kuna makosa makubwa mawili ambayo Wakristo wengi tunayafanya tuwapo katika majaribu. Na makosa haya ndiyo yanayogharimu uhusiano wetu na kutufarakanisha na Mungu. Makosa hayo ndiyo yanayofanya tunaangushwa na majaribu.
Kosa la kwanza; tunatumia akili zetu kutafuta ufumbuzi wa jinsi gani tutavuka jaribu tunalopitia kwa ushindi na kumuacha Mungu kando ambayo ndiye msaada wetu. Hapa ni lazima uelewe, Mungu pekee ndiye anayetushindia majaribu, kwa akili zetu na nguvu zetu na maarifa yetu hatuwezi kamwe kujinasua katika majaribu. Uwapo katika jaribu ni lazima umkabidhi Mungu njia zako na jaribu lako, Yeye ndiye ushindi wako kwa Jina la Yesu Kristo (2 Petro 2:9, Zaburi 37:5)
Kosa la pili; kuwaangalia wanadamu wanafanya nini na wanasema nini tunapopita katika jaribu hasa wapendwa au wakristo wenzetu. Kitu tunachojisahau hapa ni kwamba tunategemea wingi wa marafiki tunaokuwa nao wakati wa furaha ndio hao hao tutakao kuwa nao wakati wa majaribu, sivyo! Uwapo katika shida au jaribu kama kuna mkristo mwenzako atabaki na wewe hiyo ni neema tu ya Mungu, lakini wengi kama siyo wote watakuacha peke yako.
Unajua kwa nini watakuacha peke yako? Jaribu siyo lao ni lako, anayepaswa kushinda siyo weo ni wewe. Kwa hiyo ni lazima upite peke yako ili ushinde peke yako na tuzo ya ushindi utapata peke yako. Hupaswi kuwaangalia wapendwa na hupaswi kulalamika iwapo watakuacha upite katika jaribu peke yako.

Hebu tuangalie mfano; kuna wakati Yesu Kristo alizuiliwa na Wasamaria kuingia katika kijiji chao, Yakobo na Yohana walichukizwa na jambo hilo na wakataka kuagiza moto kutoka mbinguni ili kuwaangamiza Wasamaria wale lakini Yesu Kristo aliwazuia (Luka Mtakatifu 9:51-56)
Ilipofika wakati Yesu Kristo anakikabiri kikombe cha mateso, baada ya kuila pasaka aliwachukua wanafunzi wake hadi bustani ya Gethsemane na akawachukua Petro, Yakobo na Yohana kwa ukaribu zaidi. Akawaambia Roho yangu ina huzuni kiasi cha kufa, kaeni hapa mkeshe pamoja nami (muombe pamoja nami), lakini wanafunzi hawa walipofika sehemu hii walilala wakamuacha Yesu Kristo apambane mwenyewe. Kwa sababu hawakua na sehemu ya kukinywea kikombe cha mateso cha Yesu Kristo (Mathayo Mtakatifu 26:36-40)
Kwa hiyo ninataka utambue kuwa uwapo katika jaribu hupaswi kutumia akili, ufahamu, elimu na nguvu zako kujinasua kutoka katika jaribu. Mruhusu Mungu akuvushe mwenyewe kwa utukufu wake kwa jina la Yesu Kristo. Pia ni lazima wapendwa au wakristo wenzako wakuache ili uvuke wewe mwenyewe kwa sababu unayejaribiwa ni wewe na siyo wao.
Namna ya kupita katika jaribu ili upate ushindi wa heshima
Hapa ndipo penye kiini cha somo hili, namna unavyopita katika jaribu ndivyo kunaamua namna na aina ya ushindi utakao upata. Ukipita kwa akili zako utapata matokeo yanayolingana na akili yako, na hata ukishinda hutapata ushindi wa heshima wenye utukufu wa Mungu. Kwa mfano wapo mabinti wawili wanatafuta kazi, mmoja akatumia mwili wake (rushwa ya ngono) na mwingine akamtumaini na kumtegemea Mungu, wote wanaweza kupata kazi, lakini furaha ya kupata kazi na utukufu wa kazi utatofautiana na hata muda wa kudumu katika kazi utatofautiana pia.
Unapopita katika jaribu, ni lazima uzingatie mambo yafuatayo ili Mungu akupiganie na upate ushindi wenye sifa na utukufu kwa Mungu, ushindi wenye taji safi kwa imani na ushuhuda wako.
Utii kwa sauti ya Mungu
Unapokuwa na jaribu shetani huongea mara nyingi kwa sauti nyingi, lakini Mungu huongea mara chache sana kwa sauti moja tu. Ni lazima ukubali kuisikiliza, kuitambua na kuitii sauti ya Mungu, huo ndio ushindi wako.
Yoshua 6:3-4. “Nanyi mtauzunguka mji huu, watu wote wa vita, mkiuzunguka mji mara moja. Fanya hivi siku sita. Na makuhani saba watachukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume, mbele ya hilo sanduku; na siku ya saba mtauzunguka mji mara saba, nao makuhani watapiga tarumbeta zao.”
Kabla ya kufika katika mji wa Yeriko, Israeli walipigana vita vingi na kama ni ujuzi wa vita basi walikuwa nao. Wangeweza kuingia Yeriko pasipo kumshirikisha Mungu kwa sababu vita nyingi walizopigana walishinda, walikuwa na kila sababu ya kujiamini. Lakini waliamua kumshirikisha Mungu, na Mungu aliposema nao walimsikiliza na kutii sauti yake.
Watu wengi tunachokosea ni kwamba tunaomba msaada wa Mungu na wakati tunasikiliza sauti nyingine tofauti na sauti ya Mungu. Mungu anapotupa majibu, tunafuata na kutii sauti nyingine na siyo sauti ya Mungu, na hapa ndipo tunajipata tumeangamizwa.
Kwa kutii maelekezo ya Mungu, Israeli walipata ushindi wa kuuingia mji wa Yeriko kwani Mungu alifanya vita kwa ajili yao (Yoshua 6:15-16, 20).
Na wewe ukiamua kuisikiliza sauti ya Mungu na kutii kufuata maelekezo yake, hakika ushindi utakuwa upande wako kwani Mungu mwenyewe atapigana na adui zako kwa ajili yako.
Uwe na imani, Mungu atatenda
Mungu ni Mungu wa ahadi, anatenda jambo kulingana na ahadi iliyopo ndani ya neno lake. Pale tunapoona hakuna njia, kiza kinene mbele, hatuna msaada ndipo Mungu hufanya njia hapo (Isaya 43:16).
Unapokuwa katika jaribu, kadri siku zinavyoongezeka ndivyo unapaswa kuzidisha imani yako kwa Mungu. Na kama ulikuwa ukimuomba Mungu mara moja kwa siku, ongeza maombi zaidi ikiwezekana hata mara tano kwa siku. Ipo siri katika kufanya hivi, kwanza unamfanya Mungu aoneimani yako kwake inakuwa na nia yako thabiti ya kuhitaji msaada wake. Pili, ni njia ya kumdhohofisha shetani na kumfanya ashindwe vita na kukuachilia mara moja.
Ninakuhakikishia, kwa kufanya hivi ni lazima Mungu atakuokoa katika jaribu lako kwa ushindi mkubwa na haraka iwezekanavyo.
Tunza utakatifu
2 Petro 2:9. “basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu.”
Maandiko yanasema wazi, Bwana huwaokoa watauwa (watakatifu) na majaribu. Unapopita katika jaribu, kitu cha muhimu kukitunza ni utakatifu na uhusiano wako na Mungu.
Ayubu mtumishi wa Mungu aliongea kauli ngumu sana. “mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, mimi nitarudi tena huko uchi vile vile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe”. Ukiichunguza kwa undani kauli hii, utaona kuwa Ayubu hakuvitegemea vitu au mali zinazoonekana kwa macho bali alivitazamia visivyoonekana kwa macho (2 Wakorintho 4:16-18)
Na zaidi Ayubu alitaka kuulinda na kuutunza utakatifu wake na uhusiano wake na Mungu. Na ndivyo inavyokupasa mkristo, usiangalie ni vitu vingapi unavipoteza unapopitia jaribu ulilonalo, bali zidi kuimarisha uhusiano wako na Mungu ukiulinda utakatifu wako.
Kwa hiyo unapopita katika jaribu lolote ni lazima uzingatie mambo makuu matatu tuliyojifunza hapo juu, nayo ni; utii wa sauti ya Mungu, imani na utakatifu. Katika hayo, hakika Mungu atapigana kwa ajili yako na kukupa ushindi mkuu.
Nina imani umebarikiwa na kupata kitu kipya katika somo hili ambalo kupitia Roho wa Mtakatifu, Mungu ametufundisha. Shiriki baraka hizo kwa kushiriki somo hili katika ukurasa wako katika mtandao wowote wa kijamii.

Comments

Popular Posts