NGUVU YA MANENO KTK MAISHA YETU.
Katika maneno
tunayoyazungumza kuna nguvu ya uumbaji wa kile tunachokizungumza. Kwa mfano
mtumishi wa Mungu anapofanya maombezi kwa ajili ya mtu fulani, anatamka maneno
ya uponyaji kwa imani, na yule anayeombewa akiyasikia yale maneno ya uponyaji
anaamini katika maneno yale na ndipo anapokea uponyaji. Hii inatokea kwa sababu
maneno tunayoyasikia yanatufanya tujenge picha ya kile tunachokisikia. Ukisikia
maneno ya uponyaji unapata picha ya kupona, ukisikia maneno ya kukutia moyo
unapata picha ya kutiwa moyo na ukisikia maneno ya kukukatisha tamaa utapata
picha ya kukata tamaa na kushindwa. Na jambo hilo linasababishwa na jinsi
tunavyojenga imani katika maneno tunayoyasikia ama kujisemea wenyewe.
Yakobo 1:19 “Basi kila mtu na
awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema;”.
Mstari huo wa kitabu kitakatifu cha Biblia, unatufundisha
kutokuwa wepesi wa kusema. Kwa sababu katika kusema sana tutasema maneno yenye
kuvunja moyo, kukatisha tamaa, kulaani na hata maneno yasiyo na maana ili mradi
tuonekane tumesema. Tunatakiwa tuseme au tuongee maneno ya kubariki, kutia moyo
na kufariji; maneno ambayo mtu anayekusikia atatamani akusikie tena na kesho na
siku inayofuata kwa sababu una kitu cha maana katika maisha yake.
Baraka, kwa kutumia
maneno ya vinywa vyetu tunaweza kubariki. Tukitaka kumbariki mtu au kumfariji
tunatumia maneno. Tunatamka maneno yenye baraka au kufariji. Mwanzo 27:27-28 “…akambariki
AKASEMA (maneno), Mungu na akupe ya
umande wa mbingu, na ya manono ya nchi, na wingi wa nafaka na mvinyo.”
Laana, pia kwa
kututmia maneno ya vinywa vyetu tunaweza tukatamka maneno ya kulaani. Ambapo
tunaweza kujilaani wenyewe au wenzetu kwa kujua ama kutokujua. Tunapoongea
jambo baya kwa maisha yetu au ya wenzetu tunakuwa tunatamka laana ambazo ni
lazima zitatimia. Zaburi 10:7 “kinywa chake kimejaa laana, na hila na dhuluma, chini ya
ulimi wake kuna madhara na uovu.”
Ikiwa unatamka
laana au baraka, ushindi au kushindwa katika maisha yako au ya mtu mwingine, ni
lazima jambo hilo litakuja kutimia. Unaweza ukamwambia mtu fulani kuwa unataka
uanze kufanya biashara, na mtu huyo akakwambia, “na wewe unataka kufanya biashara, ameshinwda fulani utaweza wewe?”
badala ya kumjibu NITAWEZA, unamjibu
‘najaribu jaribu tu ndugu yangu’.
Unaanza biashara alafu miaka inakatika huoni faida yoyote, ni kwa sababu
uliyemshirikisha jambo lako aliongea kushindwa na wewe pia ukakiri kushindwa
huko. Kwa maana hiyo unaweza ukawa umetamkiwa/umejitamkia laana au baraka
katika maisha yako bila wewe kujua. Na falme zote mbili; ufalme wa giza na
Ufalme wa Mungu zinafuatilia unayoyakili kwa ajili ya maisha yako au ya wenzako
ili kuyatenda au kuhakikisha yanatendeka.
Isaya 59:17(a) “Mimi nayaumba matunda ya midomo;”. Hapa Mungu
alimwambia nabii Isaya kuwa yeye (Mungu), anayaumba matunda ya midomo yetu, kwa
maana nyingine ni kwamba Mungu anayaumba maneno tunayotamka kwa ajili ya maisha
yetu au wenzetu.
Na kwa upande wa ufalme wa giza pia yapo mapepo
yanayofuatilia na kutimiza maneno ya vinywa vyetu, hasa maneno ya laana ili kuhakikisha
tunaishi maisha yenye mateso na dhiki.
Kwa hiyo ndugu mpendwa katika Kristo Yesu, unatakiwa kufanya maombi ya
kufunga ili uvunje laana zote katika maisha yako, laana ulizojitamkia kwa kujua
au kutokujua na zile walizokutamkia wengine. Na Mungu yupo atakujibu na
kukubariki, muamini tu.
Comments
Post a Comment