Karama ya Imani (1Wakorintho 12:9)
Kila mtu aliyeokoka anayo
imani. Imani hiyo ni kipawa cha Mungu
(Waefeso 2:8), ni kama mbegu iliyopandwa ndani
yetu na kukua. Imani hii inaanza ndani
yetu kwa kusikia Neno la Kristo(Warumi
10:17). Imani hii inakuwa kwa njia ya
kuzidi kulifahamu Neno na kuzoezwa katika hali mbalimbali kulitumia Neno,yaani
kulitenda.
Tunaposema “karama ya Imani” ni
imani ya tofauti na ile ambayo kila mtu anayo.
Hii ni imani ‘maalum’ ambayo Roho wa Mungu ana mvuvia mtu katika
mazingira fulani ili aseme, au atende jambo lisiliwezekana kabisa
kibinadamu. Baada ya hali hiyo au hitaji
hilo kuisha mtu
hujikuta katika hali ya kawaida.
Karama ya imani ni uvuvio wa Roho,
ambao unakuja na ufahamu unaojenga ujasiri wa kusema au kutenda jambo fulani
ambalo haliwezekani kabisa! Karama hii
mara kwa mara hujidhihirisha pamoja na karama ya miujiza au uponyaji. Sikiliza ushuhuda huu:
Ilikuwa mwaka 1984 nikiwa kwenye maandalizi ya mkutano
nyumbani. Ilikuwa saa nne asubuhi. Wakati ninafanya usafi na kuandaa
chakula cha wageni ghafla kamba ya jiko la umeme ilivuta chupa iliyokuwa imejaa
chai ambayo ilikuwa tayari kwa ajili ya wageni na kuanguka chini kisha chupa
ikapasuka na chai ikamwagika, vipande vya chupa vikaonekana. Ilikuwa haina kazi tena. Nilipatwa na hasira, na kujiuliza kwa nini
hiyo chupa ipasuke wakati huo nikiwa na wageni?
Nikasema yule Mungu aliyeponya vipofu na viwete nilipokuwa kwenye huduma
aiponye hii chupa. Mmoja wa wageni
akaniambia mama si jambo la kawaida tu chupa kupasuka? Nikamwambia hapana,
nakataa jambo hilo
tangu sasa katika jina la Yesu. Wakasema
unakataaje na imeshapasuka? Nikawaambia
mimi sitambui kupasuka kwa hiyo chupa, nikaichukua nikaweka mikono juu yake,
nikasema kwa jina la Yesu aliyeponya vipofu na viwete huko nilikotoka wewe
chupa uwe mzima sasa. (ufahamu na ujasiri uliomwezesha kutamka maneno haya
juu ya chupa hii ilikuwa ni uvuvio wa Roho kwa karama ya imani). Wale wageni
wakanihurumia sana,
tena wakacheka. Wakasema huyu mama
amechanganyikiwa, nikasema sijachanganyikiwa Yesu anaponya hata visivyo na
uhai. Ghafla tukasikia kama
tetemeko mle ndani na watu wote wakajaa hofu wakanyamaza kimya. Nikawaambia ileteni chupa sasa ni nzima
nikaichukua ile chupa na kuiangalia ndani sikukuta vipande ndani bali chupa
mpya. (Kutokea kwa chupa mpya hii
ilikuwa ni muujiza, muujiza ni uumbaji wa kitu kipya, muujiza huu ulifanya kazi
na karama ya imani). Watu waliokuwepo walitubu na kulia wakisema
kama Mungu anaweza kuponya chupa isiyo na uhai
je si zaidi binadamu mwenye uhai? (Muujiza huu ulikuwa ni ishara
iliyowafundisha kwamba Mungu ana uwezo wa kuweza kumponya mtu). Hapo
hapo kulikuwa na mama mwenye ugonjwa wa pumu miaka kumi na tano akasema
nimwombee. Nikamwombea akapokea uponyaji
palepale, ni mzima mpaka leo. Kama Mungu
anaweza kuponya “themos” isiyo na uhai si zaidi sana mwanadamu?
Kuna ushuhuda mwingine ambao
utausoma katika sura inayofuata, unahusiana na mama Mbise kwa uwezo wa Mungu
kumwua nyoka kwa ngumi katika jina la Yesu.
Ujasiri aliovikwa kama utakavyoenda kuona ni karama ya imani.
Petro alipomwambia kiwete kwa jina
la Yesu simama utembee (Matendo 3:6), inawezekana Mungu Roho Mtakatifu
alimvisha ujasiri na ufahamu wa kutamka neno lile kwa karama ya imani. Maana kiwete yule alikuwepo siku nyingi
kabla, kwa nini hakumwombea siku za nyuma? pengine Mungu alijua kwamba karama
ya imani ilihitajika. Hata hivyo imani
zetu pia zinaweza kufanya mambo makubwa si karama ya imani tu, kama tutakavyo
ona katika sura za mbele.
Comments
Post a Comment