MANUNG’UNIKO HUGEUZA BARAKA ZA MUNGU MAISHANI MWAKO NA KUWA LAANA KTK MAISHA YAKO.


    Manung’uniko ni dalili ya kukata tamaa na kukiri kukosa tumani la jambo au hali ngumu anayoipitia mtu. Japokuwa mtu huyo anaweza asikiri kukata tamaa kwa kinywa chake, lakini kwa kupitia manung’uniko anakiri kukata tamaa na kukosa msaada japo siyo kwa ukiri wa moja kwa moja.
Katika maisha ya kiroho haipaswi kunung’unikia hali ya maisha au majaribu unayopitia, hasa haipaswi kumnung’unikia Mungu. Kwa sababu, kama nilivyokwisha kueleza hapo mwanzo, manung’uniko ni dalili ya kukiri kukata tamaa na kukosa mwelekeo.
Ni afadhari ujilaumu na kujinung’unikia nafsi yako wewe mwenyewe na siyo kumnung’unikia Mungu. Mtumishi wa Mungu, Ayubu alipofikwa na jaribu zito la kupotelewa na watoto, wanyama na kupata ugonjwa mbaya wa ajabu hakuthubutu kumlaumu au kumnung’unikia Mungu kwa kinywa chake au kwa moyo wake. Hebu tuangalie maandiko yafuatayo;
Ayubu 1:20. Ndipo Ayubu akainuka akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake,  na kuanguka na nchi na kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, name nitarudi tena huko uchi vile vile; Bwana alitoa na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe. Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.
Ni neno la kuajabisha sana, baada ya Ayubu kupata habari ya kupotelewa watoto wake wote na mali yake yote, alirarua joho lake, akanyoa kichwa chake, akaanguka na kusujudu.  Kwa kurarua joho lake na kunyoa kichwa chake alionesha utii na unyenyekevu mbele za Mungu. 
Ayubu alionesha utii kwa Mungu kwa sababu alijua, watoto wake na mali zake alivipata kwa sababu Mungu alimbariki vitu hivyo. Na ndani ya moyo wake, Ayubu alimsujudia Mungu kwa sababu huyo ndiye aliyebaki naye, na Mungu ndiyo tumaini na msaada wake tu.
Ayubu 3:1. Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake.
Ilipofikia wakati moya wa Ayubu ulipotaka kunung’unika na kusononeka, Ayubu aliona ni vema ailaani siku yake ya kuzaliwa lakini hakuthubutu kumlaani au kumnung’unikia Mungu wa mbinguni aliyemuumba.
Unapomnung’unikia au kumlaani Mungu kwa mambo magumu unayoyapitia au unayokutana nayo katika maisha yako, unafanya kosa kubwa sana. Ni busara endapo utamuuliza Mungu nini makusudi ya mapito haya, ili kama ni vita dhidi ya shetani, Mungu atakuelekeza jinsi ya kuvipigana na kwa Jina la Yesu Kristo utashinda kwa ushindi mkubwa.
Hebu tuangalie neno la Mungu (kutoka kinywani mwa Bwana) linasemaje kuhusu manung’uniko;
Hesabu 14:26-38. 26. Kisha Bwana akanena na Haruni na Musa na kuwaambia, 27. Je nichukuliane na mkutano mwovu huu uninung’unikiao hata lini? Nimesikia manung’uniko ya wana wa Israeli, waninung’unikiayo. 28. Waambieni, kama niishivyo, asema Bwana, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi; 29. Mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili,
30. Hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni.
34. kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arobaini, kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo miaka arobaini, nanyi mtakujua kufarikana kwangu.
Katika kifungu hicho cha Biblia hapo juu tunajifunza vitu vikuu vipatavyo vine, navyo ni kama vifuatavyo;
Manung’uniko ni uovu mbele za Mungu
“Nichukuane na mkutano mwovu huu uninung’unikiao hata lini?”, maneno hayo ya Mungu yanapatikana katika Hesabu 14:26. Maneno na mawazo yanayoambatana na manung’uniko ndiyo hufanyika uovu mbele za Mungu. Watu wengi wanapo nung’unika hutamka maneno au huwaza mawazo ya kumlaani Mungu, na wakati mwengine kuwalaani na kuwaumiza wengine. Hapo ndipo manung’uniko yanapokuwa ni uovu mbele za Mungu.
Na mara nyingi, manung’uniko yanaambatana na kukata tamaa, na kukata tamaa mar azote huwa ni chanzo cha kutenda dhambi kwa namna moja au nyingine. Kwa maana hiyo; manung’uniko huzaa kukata tamaa na kukata tamaa huzaa dhambi, dhambi ni uovu na chukizo mbele za Mungu.
Kwa mfano; mwanadamu anapo kata tamaa kutokana na ugumu wa maisha, hutafuta njia haramu ya kumuwezesha kuishi kama kufanya ukahaba, wizi na ujambazi, mauaji n.k. hayo yote huja baada ya mtu huyu kunung’unika kuhusu ugumu wa maisha, baada ya kukosa majibu hufikia kukata tamaa inayopelekea kuchukua maamuzi yasiyo sahihi ambayo ni dhambi na chukizo mbele za Mungu kama tulivyoona katika mfano hapo juu.

Manung’uniko husababisha kifo
“mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili”, Hesabu 14:29. Kuna aina mbili za vifo; kifo cha kimwili na kifo cha kiroho.
Maisha ya dhambi yanayotokana na kukata tamaa baada ya manung’uniko ya muda mrefu, hupelekea kifo cha kimwili na kiroho. Kifo cha kiroho ni kurudi nyuma baada ya kupokea wokovu wa Yesu Kristo, unapoishi maisha ya dhambi unakuwa umerudi nyuma kiroho au umeanguka dhambini. Na kifo cha kimwili hufuatia kama matokeo ya maisha ya dhambi unayoyaishi.
 Haimaanishi wasiotenda dhambi hawafi, la hasha, bali maisha ya dhambi humpeleka mtu kaburini pasi na umri timilifu (Ayubu 5:26, Ayubu 42:16-17). Yohana 8:21(b), nanyi mtakufa katika dhambi yenu. Kama tulivyoona hapo juu; manung’uniko huzaa kukata tamaa, kukata tamaa huzaa dhambi na dhambi huzaa kifo, kinachoweza kuwa cha kiroho au cha kimwili.

Kutofikia au kutotimiza malengo yako au makusudi ya Mungu katika maisha yako
“hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo”, Hesabu 14:30.
Hayo yalikuwa ni maneno ya Mungu kwa wana wa Israeli, na kama tulivyoona hapo juu; manung’uniko husababisha kukata tamaa na kukata tamaa husababisha kutenda dhambi na dhambi hupelekea mauti ya kiroho au ya kimwili au vyote kwa pamoja.
Unapokufa kiroho, unauwa makusudi ya Mungu katika maisha yako. Na Mungu asivyo na hasara wewe mmoja unaporudi nyuma, anainua jeshi kubwa la watu kumtumikia. 
Yesu Kristo alipoambiwa awatulize wanafunzi wake waliokuwa wakimsifu, na Mafarisayo; alijibu; “Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele”, hapo Yesu alikuwa akitufundisha kuwa, tunapokata tamaa na kuuwa huduma zetu, Mungu anainua watu wengine ili kuiendeleza kazi yake. Kazi ya Mungu haifi hata siku moja, ukizira wewe, atafanya mwingine, maadam utukufu umrudie Mungu.
Aidha unapokuwa na malengo katika maisha yako, kunung’unika kunakopelekea kukata tamaa inayosababisha dhambi na hatimaye kifo cha kimwili, kunazima malengo yako na kufuta kabisa ndoto zako maishani. Na kusababisha kizazi chako kifuatacho kurithi laana zako, isipokuwa kitatubu na kutakaswa kutoka katika vifungu na maisha ya laana.

Manung’uniko huchelewesha makusudi ya Mungu au mafanikio yako katika maisha
“kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arobaini, kila siku kuhesabiwa mwaka”, Hesabu 14:34
Wana wa Israeli waliipeleleza nchi ya ahadi kwa muda wa siku arobaini, waliporudisha habari ya nchi hiyo ndipo walipomlalamikia na kumnung’unikia Mungu na kusema ingekuwa heri kama wangalikufa katika nchi ya utumwa ya Misri ama wangalikufa jangwani (Hesabu 14:1-3).
Hata wewe mpendwa msomaji wangu, inawezekana uko katika wakati mgumu, unapitia majaribu mazito unayodhani huwezi kuyavuka. Unafikia hatua unakata tamaa, unamlaumu Mungu kwa nini alikuumba, ni heri ufe sasa. 
Ninakwambia sasa, acha kumlaumu Mungu, acha sasa kumlaani Mungu, acha kukata tamaa, usithubutu kurudi nyuma, kwa Jina la Yesu Kristo, yupo Mungu ili akusaidie na utasema hakika wewe Mungu umekuwa ni Ebeneza kwangu.
Ikiwa Mungu anayo makusudi na maisha yako, mafanikio yako au baraka zako ni lazima akupitishe katika kipimo cha uvumilivu na uaminifu, unapofuzu mtihani huo ndipo Mungu anapoachilia kibari katika maisha yako, huduma yako na baraka zako.
Nataka nikupe angalizo katika somo hili; siyo kila mtihani au magumu unayopitia ni makusudi ya Mungu. Muulize Mungu nini chanzo, sababu na makusudi ya hali unayopitia.
Ikiwa ni uonevu wa ibilisi, mwambie Mungu akupiganie na akupe kuyashinda yote katika Jina la Yesu Krsito.
Ikiwa ni makusudi ya Mungu upitie hatua uliyopo sasa, imekupasa kuvumilia yote, usilalamike, usinung’unike, usikate tamaa wala usimlaani Mungu. Simama imara kuitetea imani yako.
Tukichukua mfano wa wana wa Israeli, Mungu aliwapitisha jangwani katika hali ngumu kwa makusudi maalumu;
Kutoka 7:16. “Nawe umwambie, Bwana, Mungu wa Waebrania, amenituma nije kwako, kusema, wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia jangwani”,
Mungu hakuwapitisha wana wa Israeli jangwani kwa bahati mbaya, aliwapitisha kwa makusudi maalumu. Kumbuka Mungu aliahidi kuwapa nchi yenye maziwa na asali (nchi ya ahadi), ili kuifikia ile nchi, iliwapasa kupitia mtihani mzito jangwani.
Kule kuenenda kwao jangwani; kwa kumsifu Mungu aliyewatoa utumwani na sasa anakwenda kuwapa nchi ya ahadi au kwa kumlalamikia na kumnung’unukia Mungu, ndiko kuliamua ni nani ataingia na nani hataingia katika nchi ya ahadi.
Na hii ni kwako pia mpendwa mwenzangu, vile unavyomuona Mungu katika mtihani unaoupitia ndio kunaamua ni jinsi gani utafikia ahadi ya ukombozi ya Mungu iliyopo mbele yako. Ikiwa unamlalamikia, unamlaani Mungu au unakata tamaa, ni dhairi utashindwa kufikia baraka na mafanikio yako ambayo Mungu ameyaweka mbele zako baada ya kuimaliza safari ya mtihani unaoupitia, ama utaifikia kwa wakati wa kuchelewa hadi hapo Mungu atakapojiridhisha kuwa umekomaa.
Hebu tuangalie neno la Mungu kuhusu mitihani tunayoipitia; “Amri hii ninayokuamuru leo mtaishika kuitenda, mpate kuishi na kuongezeka, na kuingia katika ile nchi amabayo Bwana aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki. Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako, aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu, kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo”, Kumbukumbu la Torati 8:1-2.
Nikupe mfano mfupi; matajiri wengi wanaotumia fedha na mali zao kuwatunza yatima na maskini, historia ya maisha yao ni watu waliotokea katika hali ngumu sana za kiuchumi. Mungu anapo wabariki na kuwapa mali, anawakumbusha kule walikotokea kisha anaweka mzigo wa watu hao kumtumikia Mungu kwa kutumia fedha na mali zao katika kuwatunza yatima na maskini.
Ili Mungu akubariki baraka za kiroho ni lazima akupitishe katika mtihani wa kukataliwa, watumishi wakubwa unaowaona leo kuna kipindi kigumu walichokipitia hata kufikia hapo unapowaona wamefika na unapotamani na wewe ufikie. Wapo wachungaji walioanza kanisa na watu wa familia zao tu kwa miaka kadhaa kabla hawajafikia kuwa na wafuasi zaidi ya miatano.
Na wapo wahubiri wakubwa ambao wakihubiri maelfu ya watu wanaokoka, walianza kwa mikutano ambayo walihubiri na hakuna mtu hata mmoja aliyeokoka.
Nataka nikwambie, hawakukata tamaa, hawakumlaumu wala kumnung’unikia Mungu, bali waliendelea kumtukuza, kumuhimidi na kumtumaini Mungu katika huduma zao.
Vivyo hivyo, ili Mungu akubariki baraka za kimwili kama fedha na mali, ni lazima akupitishe katika mtihani wa dhiki ya kukosa fedha na mali. Ili akupie moyo wako una mtazamo gani kumuelekea Mungu. Ikiwa unakata tamaa, unamnung’unikia Mungu, ujue hutafikia baraka ambazo Mungu ameziweka mbele yako, na ikiwa kwa neema ya Mungu utazifikia baraka hizo, basi utachelewa sana.
Katika kumalizia, ninataka nikutie nguvu mpendwa, usikate tamaa, usimlaumu wala usimnung’unikie Mungu. Simama imara katika mtihani unaoupitia, yupo Mungu jina lake anaitwa Yehova, atakusaidia na kukutetea ikiwa tu utamtumainia na kumtegemea yeye. Hakika upo ushindi na baraka baada tu ya kuumaliza mtihani wako, usithubutu kurudi nyuma kiimani na kumuacha Mungu na wala usithubutu kukata tamaa ya maisha, shindig upo, katika Jina la Yesu Kristo. Amina.

Comments

  1. Barikiwa na Bwana umenifunza jambo asubuhi ya Leo Mungu azidi kukutumia

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular Posts