AINA ZA UPENDO.


1.      UPENDO AGAPE - UPENDO WA MUNGU. (Godly Love) 
Agape ni aina ya upendo wa ki-Mungu, utendao kazi ndani ya mtu pasipo masharti yoyote au sababu yoyote. Ni upendo usioangalia hali ya nje ya mtu. Ni  nguvu au uwezo wa mvuto wa Ki-Mungu utendao kazi ndani ya mtu, kumwonyesha mtu mwingine wema wa Mungu bila kujali hali yake yoyote. Ni upendo usio na sababu yoyote; unampenda mtu kwasababu tu unatakiwa kumpenda, nukta. Hakuna sababu nyingine. Kwa kingereza wanasema unconditional love.

Aina hii ya upendo; agape, ni kama ule aliotuonyesha Mungu kwa kuupenda. Neno la Mungu linasema ‘Mungu alitupenda tungali wenye dhambi’ (Rum 5:8) ili atuokoe na mauti itokanayo na uasi kwa Mungu. Imeandikwa katika biblia kwamba Mungu aliupenda ulimwengu wenye kila aina ya uovu, uasi na uchafu (Yoh 3:16, Rum 1:28-32) na akamtoka Kristo afe kwa ajili yetu, ili tuokolewe. Kwahiyo, alitupenda bila kujali uchafu na uasi tuliokuwa nao. Huo ndio upendo wa agape.

Mfano; Upendo wa Msamaria mwema. (Luka 10:29-37)
Msamaria mmoja alimkuta mtu mmoja asiyemfahamu, ameanguka barabarani kwasababu amepigwa ma majambazi. Huyu Msamaria aliamua kumsaidia huyu mhanga kwa kumsafisha vidonda vyake na kuchukua katika punda wake na kumpeleka katika nyumba ya wagonjwa na sii hivyo tu, bali alijitolea hata kumlipia gharama za matibabu, huu mtu asiyemjua kabisa. Huu ndio upendo wa ki-Mumgu ndani ya mtu. Hauangalii hali ya nje wala hauna masharti; bali mtu huamua kuuachilia tu kwa mtu, kawasababu Mungu ameumimina ndani yake kwa ajili ya mtu/watu wengine.

Lakini tunasoma kuwa, kabla ya huyu Msamaria kupita pale njiani na kumwuoka huyu mhanga, walipita watu wengine wawili ambao wanaaminika kuwa ni watumishi wa Mungu. Kwanza alipita kuhani wa Mungu, lakini hakutaka kumsaidia, labda kwasababu hamjui. Neno linasema, alijipitisha kando akaenda zak bila kumsaidia. Kisha akapita Mlawi, amabye pia ni mtumishi wa Mungu, lakini naye pia alijipitisha kando kabisa, akaenda zake bila kutoa msaada kwa huyu mtu, kwasababu tu ni mtu asiyemfahamu. Pamoja na udini waliokuwa nao, tunasoma kuwa, hawakuweza kumsaidia huyu mtu aliyejeruhiwa vibaya na majambazi. Ni aidha, hawakuwa kabisa na upendo agape ndani yao, au hawakuuachilia upendo agape utoke, uhudumie mtu.
Lakini cha kushangaza, akaja Msamaria (amabye ni mtu wa kabila lisilohesabika kuwa la wacha Mungu) ndiye aliyeweza kuuruhusu upendo wa Mungu wa agape umhudumie yule mhanga wa ujambazi japo hamjui kabisa. Akamsafisha viWale watumishi wa Mungu walishindwa kuuruhusu upendo agape kutoka ndani yao, kumhudumia huyu mhanga. Hawa watumishi wa Mungu tuliowasoma, walitawaliwa na upendo wenye masharti na unaoangalia kwanza hali ya nje ya mtu. Upendo agape hautakiwii kuangalia hali ya nje ya mtu, wala hautakiwi kuwa na masharti yoyote. Ni upendo wa Mungu mwenyewe alitumiminia mioyoni mwetu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu (Rum 5:8)

Sifa kuu tatu (3) za Upendo wa ki-Mungu (Agape).
        i.            Hauangalii hali ya mtu ya nje.
      ii.            Hauna masharti yoyote ya kupenda.
    iii.            Hauna kipimo au kiwango cha kupenda.
    iv.            Hauna mwisho au kikomo cha kupenda.

2.      UPENDO PHILEO – UPENDO WA KIRAFIKI. (Friendship Love)
Phileo ni upendo wa kirafiki. Huu ni pendo tofauti kidogo na upendo wa agape. Phileo ni upendo wenye sababu. Kiingereza wanasema ‘congitional love’. Ni upendo wenye sababu. Huu ndio upendo unaokuwepo kati ya marafiki. Phileo ni upendo unaoshikiliwa na kishikizo/kifungo cha ‘masharti’ fulani au ‘sababu’ fulani.  Mtu huwa rafiki wa mtu fulani ‘kwasababu’ fulani. Kuna mazingra yamewafanya watu fulani kuwa marafiki. Mazingira hayo au mashrti fulani yakivunjika kati yao, basi upendo ulio kati yao huyeyuka na urafiki wao huvunjika.

Aina hii ya upendo wa phileo ni kama ile ambayo Yesu anaisema katika kitabu cha Yohana 14:21,23. Anasema kwamba ‘mtu akinipenda, Baba atampenda, nami na Baba tutakuja kufanya makoa ndani yake’. Huu ni upendo tofauti na ule unaotajwa katika Yohana 3:16 na Warumi 5:8 ambao unasema Mungu alitupenda tungali wenye dhambi pasipo masharti yoyote. Yaani, kwa upendo agape, Mungu hakujali hali zetu za nje wala masharti yoyote. Lakini kwa upendo phileo, Mungu anaangalia kwanza kama mtu atatimiza masharti aliyoyaweka, kisha ndipo na yeye Mungu  anaachilia upendo phileo kwa mtu huyo, anakuwa rafiki yake.     


Mahali pengine Yesu alisema kwa wanafunzi wake kuwa ‘siwaiti ninyi tena watumwa bali marafiki.’ Hilo neno ‘tena’ linamaanisha kwamba, baada ya kukaa na wanafunzi wake kwa muda fulani, waliweza kufikia kiwango Fulani cha mashati alichokitaka Bwana, hata sasa wamefika katika ngazi wa kuwa marafiki wa Yesu na sio watumwa tena. Ndio maana imeandikwa pia katika kitabu cha Mithali 8:17 kuwa, ‘ninawapenda wale wanipendao …’ Hivyo phileo ni upendo wenye masharti na sababu.  Rafiki wa mtu husema ‘nampenda mtu Fulani, rafiki yangu kwasababu …’ Labda kwasababu wanasoma wote au kwasababu alimsaidia katika eneo fulani au kwasababu anatabia fulani au kwasababu wanatoka kijiji kimoja, n.k.

Mfano; Urafiki wa Jonathan na Daudi. (1Samweli 18:1-4)
Tunaona Jonathan anampenda sana Daudi baada ya kugundua vipawa vilivyo ndani ya Daudi. Tunasoma kwamba Daudi alikuwa anajua sana kupiga muziki (zeze) na kuimba zaburi kwa Mungu, kitu kilichofanya Daudi awe karibu sana na Mungu na kufunikwa na utukufu wa Mungu (upako). Hivyo Jonathan alimpenda sana Daudi kwasababu Daudi ana upako, uliomsaidia babake (mfalme) Sauli kufunguka kutoka katika nguvu za giza mara kwa mara. Hivyo Daudi akawa mtu wa msaada sana kwa familia ya Mfalme na katika serikali yake. Pasipo Daudi kuwepo karibu, mambo yote ya ofisi ya Mfalme na nyumba yake yanaharibika. Hicho kilimfanya Jonathan kumpenda sana sana Daudi. Na Daudi naye akampenda sana Jonathan kwasababu Jonathan alimpenda yeye kwanza, na pia kwasababu Jonathan alikuwa motto wa mkuu wan nchi, mtoto wa Mfalme. Kukajengeka upendo mkubwa sana wa kirafiki kati ya Daudi na Jonathan, upendo Phileo. Hivyo, Phileo ni upendo wenye sababu au masharti.

Mfano Mwingine; Urafiki wa Yesu na Lazaro, Mariam na Martha. (Yohana 11:5, 35-36)
Japo biblia haielezi wazi wazi sababu za urafiki wao, lakini maandiko yanaonyesha wazi kuwa, uhusiano wa Yesu na kina Lazaro, Martha na Mariam, ulikuwa wa karibu sana ingawa hawakuwa ndugu zake wala wanatimu wake, bali marafiki zake. Angalia inavyoelezwa katika msatri wa 5; Neno la Mungu linasema, 5Naye Yesu alimpenda Martha na umbu lake (dada yake, ambaye ni Mariam) na Lazaro (kaka yao). Hebu jiulize, kwanini Roho Mtakatifu alimwongoza Yohana kutanguliza kumuandika Martha kwanza, kabla ya Lazaro au Mariam? Hii ni wazi kwamba, Yesu alikuwa na uhusiano wa kirafiki, tena wa karibu sana na hii familia, na hasa Martha (nionavyo mimi, kulingana na maandiko). Tuangalie zaidi mazingira haya kama ilivyoandikwa.

Yohana 11:20; Martha aliposikia kwamba hatimaye Yesu amefika msibani japo kwa kuchelewa, alikwenda kumlaki (kumpokea) lakini Mariam hakutoka, alibaki ndani. Unadhani kwanini? Baada ya kuongea na Yesu kwa muda Fulani, ndipo tunamona Mariam akiamua kwenda kmwuita na Mariam, atoke ndani kwenda kumsalimia Yesu (mstari wa 28-32) Hii inaonyesha ukaribu uliokuwepo kati ya Yesu na Martha. Walikuwa na upendo mkubwa sana wa kirafiki, Phileo.

Kwa wale wasomaji wa Biblia, mnakumbuka hata wakati Yesu alipotembelea familia yao siku moja, ni Martha aliyeonyesha kumjali Yesu sana hata kujituma jikoni ili kumuandalia chakula, wakati Mariam hakuwa hata na pressure, bali alijiketisha miguuni pa Yesu kusikiliza Neno la Mungu. Japo badaye Martha alishushuliwa na Yesu, lakini ndiye aliyeonyesha kumjali (kum-care) Yesu zaidi, ndiye aliyeonyesha kusumbuka kwa ajili ya Yesu zaidi kuliko Mariam. Soma hii katika kitabu cha Luka 10:38-42.

Mimi naamini urafiki wa Martha kwa Yesu alijengeka katika mazingira ya Martha kuthamini wema na baraka alizotendewa na Yesu, kwasababu utakumbuka kwamba, Martha ndiye yule mwanamke kahaba, ambaye siku moja alisikia injili katika mkutano ambao Yesu alikuwa anahubiri na akatubu dhambi zake, akatua mzigo wake na Yesu akamsamehewa kabisa uovu wake wote. Kwa furaha aliyokuwa nayo, akaenda nyumbani kwake, akachukua chupa ya perfume (marhamu) safi tena ya bei kubwa, akaja mahali ambapo Yesu alialikwa chakulani nyumbani kwa Farisayo aitwaye Simon.

Kwa utaratibu wa kiyahudi, ni mwiko kabisa mwanamke kuingia katika kikao cha wanaume wala kumgusa mwanaume bila utaratibu. Lakini kwa jinsi alivyokuwa na msukumo mkubwa moyoni, alishindwa kujizuia, akapenya mpaka mahali walipokuwa wamekaa chakulani, akasimama nyuma ya Yesu, akadondosha machozi katika miguu ya Yesu (kwasababu wayahudi hukaa chini kwenye zulia, na hii ina maana kwamba, Yesu alikuwa amekunja miguu kwa nyuma, ndio maana machozi yakamwangukia miguuni).  

Biblia inasema, ndipo alipoinama na kuvunja ile ya marhamu safi, nyumba yote ikajaa harufu nzuri. Martha akaipaka miguu ya Yesu mafuta yale mazuri, akachukua nywele zake ndefu na kuipangusa vizuuuri miguu ya Yesu. Mwisho akamalizia kwa kuibusu sana miguu ya Yesu mpaka mafarisayo wakakwazika na kunung’unika; lakini Yesu akamtetea Martha na kusema ‘mwacheni! Huyu amesamehewa dhambi nyingi kuliko ninyi, ndio maana amenipenda zaidi sana kuliko ninyi wote. Kwa habari kamili, soma Luka 7:36-50.
Pengine kwa sababu ya unyenyekevu wa Martha, ndipo upendo wa kirafiki (phileo) ulipozaliwa kati ya Yesu na Martha. Tunasoma hatimaye siku nyingine, Martha akamualika Yesu chakulani nyumbani kwao (Luka 10:38-42). Kitendo hicho kilimtabulisha Yesu kwa familia ya Lazaro. Biblia inasema Yesu akawapenda sana Martha, Mariam na Lazaro kirafiki - phileo (Yoh 11:1-5). Baada ya hapo, ndipo Lazaro alipougua sana hata Martha akatuma watu kwa Yesu kumwomba aje kumponya kaka yao ambaye pia ni rafiki sana wa Yesu. Mpaka Lazaro anakufa, Yesu alikuwa hajatokea.

Siku Yesu anafika, walikuwa wameshamzika Lazaro siku nne zilizopita, tayari ananuka, ameharibika. Habari ziliposikika kwamba Yesu amefika msibani, ni Martha peke yake aliyetoka kwenda kumlaki Yesu. Baada ya muda Martha kuongea na Yesu kwa muda, ndipo akrudi ndani kwenda kumwita Mariam atoke kwenda kumsalimia Yesu kule nje. Mariam akatoka, naye alipomwona Yesu, alilia kwa uchungu sana na kujibwaga miguu pa yesu na kulalama ‘Yesu kama ungeuja mapema, kaka yetu asingekufa, ungemponya’.

Yesu alipomwona Mariam analia, na wayahudi waliofuatana naye wanalia, Yesu akaugua sana moyoni, akafadhaika, na mstari wa 35 unasema “Yesu akalia machozi”. Hata wayahudi walipomuona Yesu analia, waksema, “angalia jinsi alivyompenda (Lazaro)”. Hii inaonyesha kwamba, kulikuwa na upendo mkubwa sana wa kirafiki kati ya Yesu na Lazaro na dada zake. Baada ya hayo, tunasoma Yesu akaenda kumfufua rafiki yake Lazaro kutoka mautini.

Ndipo katika sura inayofuata (Yoh 12:1-8) baada ya wakati fulani kupita tangu Yesu amfufue Lazaro, tunaona familia ya Lazaro wanamwandalia Yesu karamu (sherehe au party), pengine ilikuwa ni ibada ya shukurani ya kufufuka kwa Lazaro. Siku hiyo, Martha akaanda chakula kizuri, halafu wote wakiwa wameketi chakulani, Martha akarudia tena kumvunjia Yesu kibweta cha marashi safi, kumbuka hii ni mara ya pili anamfanyia Yesu tendo hili la upendo.

Martha akamvunjia Yesu kibweta kingine cha marashi (perfume) safi ya bei kubwa; akampaka tena Yesu marhamu safi kwa nywele zake. Ilikuwa ni ratili ya mafuta safi ya marhamu yenye thamani nyingi. Safari hii Yuda ndiye aliyekwazika (soma mwenyewe utajua sababu). Lakini tunamwona Yesu akimtetea tena Martha na kusema ‘mwacheni, kwa kitendo hiki, ananiandaa kwa maziko yangu’. Hii inatuonyesha jinsi Yesu alivyokuwa na urafiki wa Karibu sana na Martha. Martha alimpenda sana Yesu kwa wema usioelezeka, ambao Yesu alimtendea yeye na familia yake. Upendo uliokuwa katika yao ni upendo phileo, Upendo wa kirafiki, upendo wenye sababu.

Sifa kuu tatu (3) za Upendo wa kirafiki (Phileo).
        i.            Unaangalii hali ya mtu ya nje.
      ii.            Una masharti yoyote ya kupenda.
    iii.            Una kiwango au kipimo cha kupenda.
    iv.            Una mwisho au kikomo cha kupenda.


3.                              UPENDO EROS – UPENDO WA KIMAPENZI AU MAHABA. (Romantic/Sexual  Love)
Eros ni upendo wa kimapenzi au kimahaba unaokuwa kati ya watu fulani kusababisha watu hao kuwa na uhusiano wa kimapenzi (mahaba) kati yao. Kwa utaratibu wa Mungu na jamii zilizo ‘sawa sawa’, Eros ni aina ya upendo unaotakiwa kuwa kati ya watu wenye uhusiano wa ki-ndoa, yaani mtu mke na mume au kati ya watu wanaoelekea katika uhusiano wa ki-ndoa wa mume na mke. Aina zote za upendo zinahusisha moyo (nafsi) wa mtu, lakini Eros huwa na sifa ya kuwa na hisia zenye nguvu zaidi toka moyoni kuliko aina zingine zote za upendo. Eros  ni aina ya upendo wenye nguvu kali sana ya hisia za binadamu.

Tunaona Neno la Mungu (katika kitabu chake maalum kinachohusu mahaba ya wapenzi wawili) kitabu cha Wimbo Ulio Bora 8:6, Neno la Mungu  linasema kwamba Upendo (Eros) huwa na nguvu sana, kama mauti. Nguvu hiyo ya upendo huunganisha nafsi (fikra,hisia na maamuzi) za wapenzi wawili kuwa kitu kimoja katika fikra, hisia na maamuzi yao kwasababu ni upendo uliolenga kujenga ndoa nzuri na familia bora.

Mfano; Upendo wa Yakobo kwa Raheli. (Mwanzo 29:10-30)
Yakobo alipomkimbia kaka yake Esau, alikimbilia nchi ya mbali, nchi ya mama yake, kwa mjoba wake Labani. Labani alikuwa na binti wawili, mkubwa aliitwa Lea na mdogo waliitwa Raheli. Biblia inasema Lea alikuwa na macho mazito, yaani ukimwangalia, utadhani amelala, kumbe ndio anakuona. Na Raheli alikuwa na umbo zuri la mwili na sura nzuri ya usoni. Na Biblia inasema kwamba, Yakobo alimpenda Raheli. (Mwa 29:16-20). Labani akamwabia Yakobo atumike kuchunga wanyama wake kwa miaka saba (kama mahari), ndipo atampa Raheli kuwa mke wake. Yakobo akapendezwa na hilo, na akakubali kutumika na kuchapa kazi za Labani kwa miaka saba ili ampate Raheli. Na Neno la Mungu linasema, kwa jinsi Yakobo alivyompenda Raheli (kwa Eros - kimapenzi kuwa mke wake), alichapa kazi sana na kwa bidii kiasi kwamba, ile miaka saba ilionekana michache sana.

Hiyo ni nguvu ya upendo Eros. Yakobo alikamatwa katika upendo eros kwa Raheli. Ilikuwa kali sana. Nakwambia eros ina uwezo wa kumfanya mtu asione ugumu wa kazi, asione machungu, asione umbali wa mwendo, asione ukali wa jua, asione aibu wala woga mbele za watu wengine; Eros ina nguvu sana juu ya mtu mwenye nayo, hata kuwatala utu wake wote. Eros ina nguvu ya fikra, hata kutawala mawazo ya mtu; eros ina nguvu ya hisia, hata kutawala kuhisi/kujisikia kwa mtu; eros ina nguvu ya maamuzi, hata kutawala matendo ya mtu kabisa. Unaweza ukamkuta kijana sik hizi ni msaaaafi kuliko tunavyomjua, kumbe ni kwasababu tayari amekamatwa kwa mwanamwali binti ‘Labani’ kama Yakobo aliyodakwa. Wee acha bwana! Tehetehetehetehe (kicheko).

Yakobo alijaa Raheli katika mawazo yake yote! Kila saa alibaki kumuwaza Raheli kwa muda mrefu; Yakobo alijaa Raheli katika hisia zake kiasi cha kutousikia machungu ya ile kazi na hata akaona miaka saba kwa si kitu kikubwa; Yakobo alijaa Raheli katika maamuzi yake hata kumfanya afanye kazi kwa nguvu kama trekta au katapila, ili tu kumpata Raheli. Raheli ndiye aliyekuwa nguvu na hamasa ya Yakobo kudamka alfajiri na mapema kwenda kulisha mifugo ya mjomba wake Labani.Upendo Eros una nguvu kama mauti aisee. Wee acha tu.

Upendo wa kimapenzi au mahaba - Eros. (Romantic Love or Sexual Love)
Upendo wa kimapenzi huwa kati ya watu wawili wanaoelekea katika uhusiano wa kudumu wa mume na mke. Mungu hakukusudia upendo huu wa kimapenzi uwe wa kujaribu na kuacha, kwasababu eros ni upendo wenye nguvu sana ya hisia (nafsi), hivyo huathiri sana moyo, ufahamu, hisia za mtu na pengine hata afya ya mwili wa mtu kabisa, kama hatajua namna ya kuutawala ipasavyo. Hivyo Eros si upendo wa kuingia na kutoka utakavyo, kama mtu abadilishaye nguo (labda kama kuna cha kujifunza; nitaeleza baadaye maana yah ii sentensi), bali eros ni upendo uliokusudiwa kukaa kati ya watu wawili tu, kwa maisha yao yote yaliyobaki hapa duniani (permanently for life), sio kuingia na kutoka, kwasababu una uwez wa kujeruhi sana myo wa mtu na kumwachia vidonda na makovu ya moyoni. Tena nasisitiza, eros ni kwa ajili ya watu wawili tu, na sio watatu au zaidi, laa sivyo huo hautakuwa upendo, bali tamaa (lust and not love). Na tena eros, ni upendo kwa ajili ya watu wawili wa jinsia tofauti tu, na sio jinsia moja.

Mfano; Upendo wa Isaka kwa mkewe Rebecca. (Mwa 26:1-11)
Isaka alikuwa akiishi katika nchi ya Wafilisti. Watu wale wakamwona Rebeka, wakavutiwa na uzuri wake, hata wakamtamani. Wakamuuliza Isaka, ‘ee bwana ee, huyu msichana tunayemwona katika boma lako na wakati mwingine unaambatana naye, ni nani kwako? Isaka akaogopa kusema ni mke wake, kwa maana wangeweza kumuua ili wamchukue Rebeka, kwa jinsi alivyokuwa mzuri wa kuvutia. Isaka akasema ‘ni dada yangu’. Basi wakamwacha. Lakini kumbe wale watu walitumwa na Mfalme Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, ili kupeleleza na kujua uhusiano wao, kwasababu Mfalme alivutiwa sana na uzuri wa Rebeka, akataka kumuao.

Siku moja, Mfalme Abimeleki alipokuwa akipta pita mitaani, akakatiza mtaa ambao nyumba ya Isaka ilikuwepo. Biblia inasema  8Abimeleki Mfalme akachungulia dirishani, akawona Isaka akicheza-cheza na Rebeka mkewe” (kimahaba/romantically). Mfalme Abimeleki akamwita Isaka, akamwambia, kwa jinsi nilivyowaona mnchezeana vile, haaaaata! lazima huyu ni mkeo, huwezi kucheza-cheza vile na dadako, sasaaaa, mbona uliniambia kuwa huyu ni ndugu yako (dadako)? Isaka akajibu ‘niliogopa nisije nikauwawa kwa ajili yake’. Basi Abimeleki akamlaumu Isaka, kwa kusema, mtu mmoja wetu angelala na Rebeka bila kufikiri ni mkeo, kwasababu ulisema mwenyewe ni dadako. Ndipo Mfalme akaamuru watu wote wasimguse Isaka wala mkewe Rebeka; akasema “11amgusaye mtu huyu  au mkewe, lazima atauawa”.

Baadhi ya Dalili na Sifa za Upendo wa Kimapenzi (mahaba) - Eros (Romantic Love).
1)      Mvuto kwa Haiba yake na kuchukuliana nayo. (Mwonekano na tabia).
2)      Kukaa mawazoni kwa mtu anayependa. (Kujaa moyoni)
3)      Shauku kubwa ya kuwa pamoja kila wakati. (Kuambatana)
4)      Heshima kubwa kwa mtu apendwae (Utii na Uaminifu)
5)      Kumjali na kumtanguliza mtu apendwae. (Kipaumbele)
6)      Zawadi na gharama kwa mtu apemdwae. (Kujitoa/Sacrifice)
7)      Furaha na Amani kutawala moyoni. (Kuridhika)


1.    The person catches your attention as you very much admire her/him.
2.      The person fills your heart and mind most of the time.
3.      You always like to be with him/her and spend time together.
4.      You always want to communicate when he/she is away.
5.      You have absolute care, kindness and concern about her/his life.
6.      You easily make sacrifices, incur costs or get gifts for her/him.
7.      You have total obedience, faithfulness and respect over her/him.
8.      You have sweet loving words of kindness towards her/him.
9.      You have a desire to express love, care and concern by touch.
10.  You have Total Peace and Joy filling your heart over her/him

Baadhi ya maandiko yanayotaja upendo eros. (Upendo wa kimapenzi)
(Waefeso 5:25.) Enyi waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake. (Mhubiri 9:8-9.) 8Mavazi yako yawe meupe siku zote; wala kichwa chako kisikose marhamu. 9Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote za maisha yako ya ubatili uliyopewa chini ya jua. (Wimbo Ulio Bora 7:1-10) 10Mimi ni wake mpendwa (mpenzi) wangu na shauku yake ni juu yangu. (Wimbo Ulio Bora 4:1-7) 1Tazama, u mzuri mpenzi wangu, u mzuri, macho yako…nywele zako… 7Mpenzi wangu u mzuri pia, wala ndani yako hamna hila.

4.                              UPENDO STORGE – UPENDO WA KIFAMILIA. (Family Love)
Upendo storge ni upendo wa kifamilia, ni upendo unaotokana na damu moja ya undugu. Ndugu wa damu moja hata kama hawapatani au wemegombana, bado ndani yao kuna upendo wa kindugu. Fikiria; mtu na mdogo wake wakiwa wamegombana sana na kutupiana mito ya makochi na vitabu vyote vya kwenye shelfu za kabati, baadaye, mmoja akimkuta ndugu yake anaonewa au anagombana au anapigwa na muuza machungwa wa mtaani, huyu ndugu yake kwa vyovyote ataguswa tu, ataonyesha kujali tu au anaweza hata kuweka tofauti zao pembeni na kuingilia kumsaidia. Msukumo huo au mvuto huo, ni mvuto unaotokana na viini vya upendo wa kifamilia unaowafungamanisha watu wa damu ya familia moja au ukoo mmoja.

Mfano; Upendo wa Musa kwa Mwebrania mwenzake. (Kutoka 2:11-12)
Musa aliona mwebrania mwenzake akipigwa na mmrisri. Kwasababu na yeye alikuwa mwembrania, ndani yake kukachemka mvuto wa kindugu, kuliwaka moto wa upendo wa kifamilia. Akainuka na kwenda kumpigania. Musa akamuua yule mmisri na akamwokoa yule mwebrania. Japo hawajazaliwa tumbo moja, lakini waote wana damu za kiebrania, na viini vile vya asili yao, viliwafungamanisha katika pendo la kindugu (kifamilia) hata wakasaidiana. Upendo huo ulimnyima Musa kujikausha wakati ndugu yake anaonewa, anapigwa na anataka kuuwawa. Si ajabu wakati anayatazama yale maonezi kwa mbali, hata alipojidai kuondoka bila kumsaidia, yamkini miguu yake ilishindwa kutembea, nafsi yake ikakamatwa kurudi kumsaidia ndugu yake. Hiyo ni nguvu ya upendo storge, upendo wa kindugu.

Mfano; Upendo wa Baba kwa Mwana mpotevu. (Luka 15:11-32)
Tunasoma jinsi mwana huyu mdogo wa baba tajiri alivyoomba sehemu ya urithi wake na kutokomea nchi za mbali kwenda kutafuta maisha. Lakini maandiko yanaeleza jinsi alivyovutwa na dunia na kuharibu mtaji wake wote wa mali alizopewa na babaye.neno la Mungu linasema, kijana huyu alijiingiza katika anasa za dunia na mwishowe alifilisika kabisa. Baada ya muda wa mahangaiko alipata kibarua cha kulisha nguruwe wa mtu mmoja. Hali yake ya kimaisha ilikuwa mbaya sana hata akatamani kula chakula cha nguruwe. Lakini akili zikamrudia na akaona anateseka bure wakati kule kwao, baba yake ana watumishi wanaokula vizuri kuliko yeye. Ndipo alipoamua kurudi nyumbani kwa toba.

Kwa hali ya mzazi wa kawaida, huyu kijana angepewa adhabu kali sana; lakini kinyume chake, baba yake mzazi alimpokea kwa shangwe na furaha. Akamvika na mavazi mazuri, akamchinjia na ng’ombe mnono na kumfanyia sherehe kuuuubwa ya kufana. Hiyo ni nguvu ya upendo wa kindugu. Japo alichofanya si cha kupendeza, lakini nguvu ya upendo wa kindugu unaweza kufunika uovu wooooote uliotendwa na ndugu yenu. Watu wanaweza kuamua kusamehe au kufumbia macho makosa yaliyotendwa na ndugu yao kwasababu ya nguvu ya upendo wa kindugu, unaitwa kwa kiebraia storge.

Upendo wa kindugu, storge  unafanana kwa sehemu na ule upendo wa ki-Mungu wa agape.
  1. Hauangalii hali ya nje ya mtu.
  2. Hauna masharti ya kupendwa.
  3. Hauna kikomo au mwisho wa kupendwa.

Tofauti yake moja kubwa na upendo wa agape ni kwamba, upendo wa kindugu una kiwango au kipimo cho kupenda. Ndugu wanapendana lakini kwa viwango tofauti; upendo wao haulingani. Tofauti ningine kubwa ni kwamba, kwasababu huu upendo wa kindugu unatokana na binadamu, basi ni lazima hautakosa madhaifu mengi. Ingawa ndugu wanaweza kuwekeana masharti fulani fulani ya kitabia ili kuweka uelewano kati yao, hata masharti hayo yakivunjwa, na baadhi ya ndugu wakasema wamefika mwisho, hawataki tena kumsaidia, lakini mwishoni, baada ya hasira kutulia na muda kupita, utaona ndugu wanainuka, wanajikongoja, kwenda kumsaidia tu ndugu yao. Hiyo ndiyo nguvu ya upendo wa kindugu au kifamilia.










NAMNA YA KUPATA MWENZI MZURI WA MAISHA.
(HOW TO FIND/GET A GOOD MARRIAGE PARTNER)
*Mithali 19:14, 21

1.      Mweleze Mungu vizuri, zile haja za moyo wako. (*Fil 4:6-7)
Mungu ameahidi kuwa atakupa mtu wa kufanana na wewe (Mwa 2:18). Kwa hiyo ni muhmusana ujijue wewe ukoje, kisha ndipo utaweza kumweleza Mungu na kumwomba akupe mtu wa haja ya moyo wako. Hivyo ni muhiu sana kujijua, kujitambua na kujielewa kwa jinsi ulivyo na ni aina gain ya watu ambao wewe unaendana nao (mnaiva). Hii ni kwasababu, watu tuko tofauti. Unaweza kuishi na mtu yoyote duniani, lakini hutaweza kuishi vizuri na kila mtu. Maisha mazuri yanakuja  kwa kukutana na mtu ambaye mnaelewana na mnaendana. Ndio maana Mungu alimwambia Adam kwamba, mwenzi wako wa maisha, atafanana na wewe.

Usimfiche Mungu moyo wako. Kumbuka, yeye ni Baba yetu na sisi tu watoto wake vipenzi. Hivyo Mungu anaheshimu sana haja za moo wako ambazo zitakupa wewe furaha ya maisha. Mathayo 7:7-11 inasema, Ombeni nanyi mtapewa. Mwana akiomba mkate, hapewi jiwe, akiomba samaki, hapewi nyoka. Anapewa alichoomba. Lakini pia ni muhimu ujue kwamba, mwana akiomba mkate, hapewi jiwe, lakini pia hapewi keki hata kama ndani ya nyumba kuna keki. Mwana akiomba samaki, hapewi nyoka, lakini pia hapewi kuku, hata kama ndani ya nyumba kuna kuku wengi. Hii ni kwasababu, Mungu anaheshimu sana matakwa na mahitaji ya watoto wake, maana anapenda kuiona furaha ya watoto wake. Soma Zab 145:17-18 na Isa 45:11 uone. Pia  1Kor 7:39.

Maombi yako ya bidii yatampa Mungu kumchonga, kumuandaa. Kila mtu huumbwa na Mungu vizuri, lakini Neno linasema kwamba, dhambi iliharibu utaratibu mwingi sana wa Mungu duniani. Soma Mwa 6:5-8 na Rum 1:28-32. Dhambi imevuruga mambo mengi sana, nafsi za watu wengi ziko corrupted (zimeharibiwa na kuvurugwa) na dhambi. kwahiyo, maombi yako yatamfanya Mungu kuanza kumshughulikia na kumtengeneza huyo mwenzi wako, popote alipo duniani. Na Biblia inasema kwamba, maombi ya mwenye haki yanafaa sana, mt akiomba kwa bidii. Soma  Yak :16,  Luk 18:1,  Kol 4:2.
2.      Mwombe Mungu akuonyeshe au akukutanishe na mwenzi wako. (*Yer 33:3)
Kila mmoja wetu ambaye Mungu amempangia kuwa na mwenzi, ana mwenzi huyo mahali Fulani hapa duniani. Pointi ya kwanza inahusu kufanya maombi ya kumwmba Mungu kumchonga na kumfinyanga huyo mwenzi wako popote alipo. Point hii ya pili inahusu kumwomba Mungu kusababisha mazingira ambayo yatawakutanisha na mtatambuana baada ya kupata ufahamu wa Mungu kwamba ‘you belong together’ yaani mnaendana, mnafanana, mnafaana na hivyo mnaweza kuishi pamoja vizuri. Hiyo ndiyo maana halisi ya kufunuliwa au kuonyeshwa. Japo Mungu anaweza kukupa maono katika ndoto au katika maombi, lakini si lazima iwe hivyo. Si kila mtu anaweza kupata maono kuhusu mwenzi wake. Soma Efe 1:15-19, Zab 32:8,  Isa 43:26,  Isa 45:11

3.      Tengeneza marafiki. (*Mith 18:24, Mith 17:17)
Watu weng humwomba Mungu kwa uaminifu sana ili wapate mwenzi wa maisha. Lakini wanfanya makosa ya kujifungia katika kisiwa cha upekee. Ni ngumu sana kuonekana na kujulikana tabia na utu wako wa ndani kama hutachangamana na jumuiya za marafiki. Mungu ndiye chanzo cha urafiki. Hat Yesu alikuwa na marafiki wa kiume na waki kike pia. (Yoh 11:5).  Jithidi kufanya marafiki mvalimbali ila mwombe Mungu akupe marafiki wazuri.

Kuna aina nyingi za marafiki; Kuna arafiki wa mbali (peer friends), marafiki wa kawaida (casual friends), marafiki wa karibu (close friends or best friends) na marafiki wa moyoni (intimate friends). Unaweza ukawa na marafiki wa kawaida wengi uwezavyo, haina shida. Lakini unahitaji marafiki wa karibu wachache (Mith 18:24). Katika wingu kubwa la marafiki zako, Mungu ataanza kukuongoza nawe utawachuja na kuwaweka katika ngazi hizo mbalimbali. Katika hali ya kawaida, Mungu atakukutanisha na mwenzi wako wa maisha kati ya marafiki zako na watu unaofahamiana nao. Kwa maombi unayofanya, Mungu atasababisha mkutane, mfahamiane, mtambuane na mptane.




  1. Thibitisha moyo wako kwamba unampenda kikweli.  (*Mhubiri 9:8-9a)
Kadri unavyoendelea na maisha ya uaminifu katika wokovu, maombi, kujifunza neno la Mungu na kumtumikia Mungu kwa namna mbalimbali, Mungu atasababisha ukutane na mtu anayefanana sana na haja za moyo wako kuhusu mwenzi wa maisha. Utahitaji usikivu mkubwa wa rohoni ili kuambua ni aina gani ya upendo unaingia moyoni mwako kuelekea kwake (kwasababu kuna aina nne za upendo). Upendo wa Mungu, Upendo wa Kindugu, Upendo wa Kirafiki, Upendo wa Kimapenzi (mahaba).

Katika ya watu unaofahmiana nao, yupo mmoja ambaye atakuwa wa tofauti sana ndani yako. Mungu atampa kuonekana watofauti sana kuliko wengine wote wanaokuzunguka. Hivyo kabla ya kwenda kusema naye na kumshirikisha uonavyo wewe moyoni mwako, thibitisha kimaombi tena na tena kwamba ndani yako kuna upendo wa kweli kwa ajli yake.  Mk 5:25 – (30) – 34; inasema, wengi walimgusa Yesu na kumsukuma-sukuma, lakini ni mmoja tu ambaye atakuwa na mguso wa tofauti katika moyo wako.

ISHARA ZA KUTAMBUA (UPENDO WA) PENZI LA KWELI.
1.      Mtu huyo atakamata umakini wako na atakuvutia (attention).
2.      Atajaa moyoni na mwazoni mwako kuliko kawaida na wengine.
3.      Utatamani sana uwepo wake wakati wote (kuwa naye).
4.      Utapenda kuwasiliana naye mara kwa mara (kama hamko wote).
5.      Utakuwa na moyo wa kumjali, wema, zawadi na kujitoa sana kwa ajili yake.
6.      Utakuwa na heshima ya juu sana, adabu, utii na uaminifu sana kwake.
7.      Utakuwa na maneno mazuri, maneno laini, na maneno ya upendo kwake.
8.      Utakuwa na moyo/uwezo wa kumvumilia au kuchukuliana naye vile alivyo.
9.      Utakuwa na hamu ya kumgusa au kumshika kwa upendo (si tamaa).
10.  Utakuwa na moyo na utayari wa kumlinda na kumhifadhi.
11.  Uhusiano wenu utapendeza mbele za watu wengi (si lazima wote)
12.  Utakuwa na amani na furaha ya ajabu moyoni mwako/mwenu.


Mungu alisema kwa mkono wa Mtume Paulo kuuelezea Upendo kwa namna hii;
1 Cor 13 : 4-8(a)
*          Upendo huvumilia/subira  (Love is patient)
*          Upendo hufadhili/hufanya wema             (Love is kind)
*          Upendo hauna husuda (Love doesn’t Envy)
*          Upendo haujivuni (Love is not proud)
*          Upendo haukosi adabu (Love is not rude)
*          Upendo hauna ubinafsi (Love is not selfish)
*          Upendo hauna uchungu (Love is not easily angered)
*          Upendo hauhesabu mabaya (Love doesn’t count wrongs)
*          Upendo haufurahii uovu (Love doesn’t rejoice with evil)
*          Upendo hufurahia ukweli (Love rejoices in truth)
*          Upendo unalinda (love always protects)
*          Upendo huamini yote (Love always trusts)
*          Upendo hutumaini (Love always hopes)
*          Upendo hustahimili (Love always perseveres)

5.  Omba ushauri kwa watu wanaokujua/wanaomjua huyo umpendaye.
2Kor 13:1;    Zab 73:24;     Mith 15:22
Ushauri kutoka kwa watu werevu wanaomjua Mungu na wanaowajua ninyi wawili utakuhibitishia kwamba ulichsikia mooni juu ya huyo mtu ni sahihi. Wakati mwingi (si wakati wote) watu wa pembeni huwa na uwezo wa kuona vizuri zaidi mambo kuliko watu mlio ndani. Wanaweza kuona vitu ambavyo ninyi mlio ndani ya urafiki hamuoni bado.washauri wanaweza kutumiwa na Mungu kuthibitisha mawazo uliyo nayo na mipango uliyonayo. Mashauri ya watu yanaweza kukusaidia kufanya maamuzi magumu nay a muhimu. (Math 18:16;   1Tim 5:19;   Ebr 10:28)

Mwombe Mungu akuongoze kwa watu wazuri wenye hekina watakaokushauri. Lakini la muhimu kuliko vyote ni wewe mhusika kubaki na uamuzi wa mwisho. Washauri wabaki washauri na sii waamuzi; wewe ndiwe uwe mwamuzi wa mwisho. Ni muhimu kupima ushauri wote unaopewa kwa maombi na uongozi wa Mungu. Wakati mwingine, Mungu anaweza kukuongoza kitu ambacho hakuna mtu mwingine anakiona ukionavyo wewe. Neno la Mungu linasema, amani ya Kristo itakusaidia kufanya maamuzi mazuri.
Soma; Fil 4:6-7, Kol 3:15 na Isa 55:12

6.  Mwendee na Useme naye kwa hekima.   (*Wimbo 3:1-4)
Baada ya maombi na subira, Mungu akuongoze kusema naye kwa wakati utakaoongozwa na Mungu. Uwe jasiri na muwazi. Lakini usemi wako uwe wa kawaida (simple). Usichague maneno magumu wala misamiati wala mafumbo. Uwe wazi na wa kawaida. Usitumie maneno ya kiroho saaaaana ili kumtisha au kumfunga mtoto wa watu. Kwa mfano; usitumie maneno kama, ‘Mungu ameniambia’ au ‘Asema Bwana wa majeshi’ maneno kama haya, yanamfunga mtu kusema “ndiyo” (kama atashitushwa nayo na kuogopa) lakini kama ni mtu jasiri na hajakupenda/hajakukubali, mtapambana. Huo sasa si mwelekeo mzuri.

Kijana mmoja alipoataliwa, akaanza kuporomosha maneno makali mfano ‘nakuzungushia ukuta wa moto, hutaolewa na mtu mwingine ila mimi, na ukikataa, Bwana atakutandika’. Hii si hekima ya Mungu. Mungu hatumii nguvu bwana. Ikiwa kwenda mbinguni tuu, Mungu halazimishi watu, Je itakuwa ndoa? Wewe ukishasema mameno rahisi; Kwa mfano; ‘nimeomba kwa muda, na hivi ndivyo ninavyosikia moyoni mwangu kwamba, nakupenda sana, na ikiwa itampendeza Mungu na wewe pia, basi uwe mwenzi wangu wamaisha’. Ukishamwambia maneno hayo rahisi (au yanayofanana na hayo) amini kwamba kama ni mpango wa Mungu muwe wote maishani, maombi yako na neema ya Mungu vitamsaidia kufanya uamuzi mzuri kwa ajili yenu wawili. Unaweza kupata jibu la ‘ndiyo’ au ‘hapana’ au ‘subiri’. Mtu wa Mungu huongozwa na Mungu, halazimishi wala hakasiriki ovyo kwa kitu kama hiki. Maana yangu ni kwamba, hauhitaji kutumia nguu ya mwili wala akili (kuwaza sana). Baada ya kuongea na kutua mzigo wako kwake, pumzika naumwachie Mungu kumalizia kazi.
    
Mkumbuke Mariam mama wa Yesu, japo alijua ana mchumba, lakini malaika aliposema naye kuhusu kupata ujauzito kabla ya ndoa, hakukurupuka mbio kwenda kwa Yusufu na kuanza kumwelesha, bali alimwachia Mungu kuongea na Yusufu. Mimi binafsi naamini Mariam alimwombea sana Yusufu. Lakini kwasababu ulikiwa mpango wa Mungu wa kuwa pamoja maishani, Mungu hakuongea na Mariam peke yake; aliongea na Yusifu pia. Mungu ni Mungu wa utaratibu, usimfundishe kazi. Jifunze kupumzika ndani ya Mungu na kutokuwa na wasiwasi. Huko ndiko kukua kiroho. Amani ya Kristo ikuhifadhi.

7.    Thibitisha uhusiano wako/wenu (kiofisi).  (*Wimbo 3:4)
Baada ya kuongea na kulitafakari pamoja kwa muda mtakaoona unatosha au unafaa, ni muhimu sana sasa mpelekane mbele, katika mamlaka zenu za kifamilia na kikanisa. Uhusiano mzuri usiwe wa mafichoni. Tunaona huyu mpenzi katika kitabu cha Wimbo anasema, anataka kumtafuta mpenzi wake, amshike mkono, wapelekane kwa wazazi. Huo ndio utaratibu mzuri kibiblia. Familia na kanisa watawasaidia kufuata taratibu za kiutamaduni na kiroho ili mhalalishwe kuwa mume na mke. Ndipo ndugu na marafiki mtawashirikisha mipango yote ili kuandaa harusi na makazi.  





Comments

Popular Posts