KUSAMEHE NI KUTII AMRI YA MUNGU!



SOMO: - MSAMAHA
Tukisoma kitabu cha WAEFESO 4:31,32 tunaona Biblia Takatifu inasema kwamba:
"Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, MKASAMEHEANE kama na Mungu katika Kristo ALIVYOWASAMEHE ninyi." (Efe 4:31,32)
Je! Nini maana ya neno MSAMAHA na kuna faida zipi katika KUSAMEHE; na kwa nini tunapaswa KUSAMEHE?
MSAMAHA:
Neno “MSAMAHA” ni neno jepesi kulitamka lakini ni pana sana katika maana. Nisemapo "NI NENO JEPESI KULITAMKA" ninamaanisha kulitamka tu kwa kawaida na katika hali ya kawaida tu pasipo kukosewa, lakini kwa watu wengi; neno MSAMAHA ni neno gumu sana kulitamka toka rohoni mwao hususani pindi wanapokosewa. Nilifanya utafiti juu ya hili neno nikagundua zipo siri kubwa sana katika KUSAMEHE ambazo Shetani apendi watu wazifahamu.
Tukirudi kwenye neno “SAMEHE” maana yake ni: Kukoma / kuacha kuhisi hasira juu ya mtu ambaye amekuumiza, kakukwaza au kakuudhi; Pia, kukoma / kuacha kuhisi hasira juu yako wewe mwenyewe (kuto kujichukia).
Neno MSAMAHA, kwa maana nyepesi linamaanisha kama ifuatavyo;
Þ       Kutolipiza kisasi japokuwa unayo haki ya kulipiza kisasi.
Þ       Ni tendo la imani na tena la hiari kwa kuwa unayo sababu, uwezo, na haki ya kulipiza kisasi kutokana na yale uliyo umizwa.
Je! Unafahamu ni kwa nini watu wengi ni wagumu KUSAMEHE?
Watu wengi hushindwa kusamehe kwa sababu hawana Roho Mtakatifu ndani yao; kwamba, wameruhusu maisha yao kutawaliwa na Shetani. 
Dhana hiyo inao ukweli mkubwa ndani yake na pia wapo watu wajiitao watumishi wa Mungu lakini nao wanashindwa KUSAMEHE. Si kwamba tu tunasamehe ili na sisi tupate kusamehewa; La, si hivyo tu, bali zipo faida nyingi sana zipatikanazo kwenye KUSAMEHE.
Siku zote mtu anapokosewa, ndani yake anazaa UCHUNGU, asipokuwa makini nao UCHUNGU unazaa CHUKI, na pia hasipojiadhari hiyo CHUKI inazaa HASIRA. Na hapo ndipo Shetani anapata mlango wa kumwingia mtu. Vitu hivyo vitatu; yaani, UCHUNGU, CHUKI na HASIRA mara zote huandamana. Usipoweza kuudhibiti UCHUNGU, unakuwa unaweka wazi mlango wa Shetani kukutawala.
Mtu kuokoka haimaanishi ndiyo mwisho wa makwazo na majaribu mbalimbali, bali tambua unapo mpokea Yesu Kristo awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako unakuwa umetangaza vita dhidi ya Shetani na majeshi yake ya pepo waovu. Shetani atajaribu kukuingia moja kwa moja, lakini akishindwa, anatafuta mbinu ya kumuingia mtu mwingine ili akukwaze; nawe ukikwazika ndipo Shetani anapata nafasi ya kukuingia na kukutawala kupitia UCHUNGU, CHUKI, na HASIRA.
Tumeona mifano mingi ya watumishi wa Mungu walio anguka kiimani kwa kushindwa KUSAMEHE; Huduma nyingi za kuhubiri Neno la Mungu zimekufa kwasababu ya KUTOSAMEHE; Makanisa mengi yamevunjika na kutengana kwa sababu tu ya KUTOSAMEHE; Ndoa nyingi na uchumba mwingi umevunjika kwasababu ya KUTOSAMEHE; Makampuni mengi yamevunjika kwa sababu ya KUTOKUSAMEHE, utaona mkurugenzi amekwazana na meneja alafu kampuni inapoteza muelekeo, utendaji unakuwa mbovu na hatimae kampuni inakufa. Yote hayo unaweza kukuta chanzo chake ni KUTOSAMEHE.
Siku zote unapokwazika Shetani anakuwa anakuletea hati ya mashtaka kwenye mawazo yako; utasikia siuti ikikwambia;
"YAANI FULANI AKUFANYIE HIVI KABISA ALAFU UMSAMEHE? HAPANA !!! LAZIMA UMKOMESHE. HAIWEZEKANI UMSAMEHE HIVI HIVI TU WAKATI AMEKUPA HASARA YOTE HII.”
 Ndipo nawe waweza ukajikuta yanakuingia akilini na ukaanza kusema: “Kweli; HAIWEZEKANI KABISA, TENA YAANI, ATANITAMBUA MIMI NI NANI."
Utaona Shetani anakukumbushia tukio jinsi ulivyo tendewa. Utasikia ushauri mwingi sana ndani ya fahamu zako. Tena maneno hayo yanaweza kukupa UCHUNGU sana kiasi cha kushindwa kula, na hata ukatokwa na machozi. Na akili ya mwanadamu ni rahisi kunasa mabaya kuliko mema; ni rahisi kukumbuka mabaya kuliko mema; hapo ndipo Shetani huchukulia point endapo usipokuwa makini. Ukimruhusu Shetani katika akili zako; ndipo utajikuta ukimtazama aliyekukwaza ni mtu wa karibu sana nawe, ambae ulitegemea angekuwa msaada kwako lakini amekurudisha nyuma na kuuumiza sana moyo wako. Hauna raha, amani wala matumaini yoyote yale. Yawezekana akawa ni rafiki yako wa karibu sana amesababisha ufukuze kazi kwa kosa ambalo hukulifanya. Kweli inauma sana; inaleta huzuni na uchungu ukiwaza utafanya nini na wale wanaokutegemea. Inaumiza sana.
Kwa wakati huo, ukijitizama uwezo wa kumdhuru unao, sababu ya kumdhuru unayo, na nia ya kumdhuru unayo. Na kila mtu unaemsimulia anakwambia:
"Mbona wewe mjinga hivyo? Ingekuwa ni mimi, kamwe siwezi kumlazia damu huyo, lazima angenitambua."
Kwa wakati huo moyo wako umejaa UCHUNGU, CHUKI na HASIRA. Lakini kwa mbali saaaana, unasikia sauti ndani ya moyo wako ikisema: MSAMEHE.
Nadhani ata wewe waweza kutambua ni jinsi gani ilivyo vigumu kuitii hiyo sauti isemayo SAMEHE kwa kuwa ukitazama ni kweli umeonewa, uwezo wa kulipa kisasi unao, na hata ukilipa kisasi au kudhuru wapo watu watakaosema "Kwa kweli umefanya vizuri kumkomesha. Ilimpasa hivyo."
Na kama ukitenda jambo baya juu yake; fahamu kwamba hiyo imetokana na wewe kuruhusu UCHUNGU ukutawale. Wengine hufikia hata hatua ya kujinyonga. Mawazo yatakujia; “Yaani fulani kabisa azini na mke wangu ! Tena fulani ni rafiki yangu kabisa ! Hapana. Lazima nimkomeshe.”
Hayo yote chanzo chake ni UCHUNU uliouruhusu uingie ndani ya nafsi (akili) yako. Tumeona Biblia Takatifu inatuambia kwamba: "Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu..." (Efe 4:31) Sasa; je! Nini maana ya neno UCHUNGU? Nivigumu kupambana na adui kama hatumfahamu adui yetu UCHUNGU ni nani.
UCHUNGU:
Kwa maana nyepesi neno UCHUNGU maana yake ni hii:
Þ       Ni hali ya kutokuwa na furaha, kujawa hasira zilizotokana na kutendewa mabaya.
Þ       Ni hali ya kuhisi huzuni nzito ambayo wakati mwingine inaweza kuchangamana na maumivu makali katika fahamu za mtu, ambayo yaweza kusababisha mwili kunyong'onyea na kusababisha akili kupoteza uwezo wa kufikiri vizuri.
Mara nyingi UCHUNGU husababisha akili kushindwa kufanya kazi ipasavyo. Hiyo ndiyo maana halisi ya neno uchungu. Zifuatazo ni athali za kutosamehe;
MADHARA YA KUTOSAMEHE:
i/: KUHARIBU AFYA YAKO.
Kama nilivyojifunza hapo awali; UCHUNGU husababisha huzuni nzito. Hii huzuni inapomwingia mtu, huleta maumivu makali katika fahamu za mtu; Uwezo wa mtu wa kufikiri vizuri hupotea, na wakati mwingine huyu mtu anakuwa kama vile amedumaa akili. Unaweza hata ukamwuliza: “Jina lako ni nani?” Lakini mtu huyo badala ya kukujibu akabaki anakushangaa tu.
Uchungu unapomwingia sana mtu unaweza kumfanya apoteze hamu ya kula. Atahisi kila aina ya chakula kwake ni kibaya, atahisi vyakula vyote kwake havina radha. Na hata akijilazimisha kula ataona kama chakula ni kigumu kumezea. Matokeo yake, afya inaanza kuzorota na mwili unaanza kunyong'onyea. Ndipo chanzo cha madonda ya tumbo. Uchungu utokanao kwa hasira husababisha mwili uweze kuzalisha sumu ambayo inaleta madhara katika afya yako.
Pia, UCHUNGU husababisha mtu kuwa na mawazo yenye maswali yasiyo na majibu kwa wepesi; na tena tumaini huonekana kama vile limepotea kabisa. Uchungu huo ukidumu kwa muda mrefu husababisha mwili kutengeneza sumu itakayoharibu ule ute mwepesi unaopatikana katikati ya mifupa (Synovial fluid) pamoja na kuharibu afya yako kwa ujumla (Bila shaka hapa madaktari wananielewa vizuri.) UCHUNGU huo ukizidi kupita kiasi, mwili wa mtu huyo huonekana umekakamaa kakamaa sana. Na kwa kiasi kikubwa afya ya mtu huyu huanza kuharibika hatua baada ya hatua. Mwili wake hunyong'onyea na akili zake hushindwa kufanya kazi vizuri, hupoteza kumbukumbu na utambuzi wa mambo mbali mbali na kumfanya mtu afanye maamuzi ya pupa yanayompeleka kwenye hasara kubwa zaidi badala ya kuleta suluhu la matatizo yake.
Hivyo basi; Athali ya pili ya KUTOSAMEHE ni kama ifuatavyo:
ii/: KUTENGWA NA WATU.
KUTOKUSAMEHE kunasababisha GHADHABU na HASIRA. Na hivi vyote hutokea pale unaposhindwa KUUDHIBITI UCHUNGU USIKUTAWALE. Mlango mkubwa wa DHAMBI huanzia pale mtu anaposhindwa kudhibiti UCHUNGU. Kwa hiyo; UCHUNGU unapomtawala mtu, uchungu huo unazaa kitu kinachoitwa CHUKI. Ndani ya hii chuki ndimo kunakaa GHADHABU. GHADHABU ni hali ya mtu kuwa na maamuzi ya pupa pasipo kujali madhara yake. Hali hiyo yaweza kumfanya mtu kuwa na majibu ya mkato mkato, kutopenda kuulizwa ulizwa; humfanya mtu kuwa na hali ya UGOMVI mara kwa mara, kutopenda kuwa na subira (anataka afanyiwe vitu kwa haraka haraka la sivyo ananuna na kutoa maneno machafu, na wakati mwingine anakuwa na tabia ya kuzira). Katika hatua hii ndipo kunazaliwa kitu kiitwacho HASIRA. HASIRA umfanya mtu kuchukua maamuzi pasipo kujali. Mtu huyo kwa wakati huo anakuwa hatarini sana kuingiliwa na Shetani. Endapo asipodhibiti hiyo hasira yawezekana Shetani akamwendesha kama jinsi Shetani apendavyo. Hapo ndipo utaona MAGOMVI, MATUSI na KILA AINA YA UBAYA vinadhihirika kwa mtu huyo. Tena anafanya pasipo hata kujali. Mtu hukirihusu hasira ikutawale utakuwa umempa Shetani kibali cha kukutawala. Biblia Takatifu inasema kwamba:
"Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira nyingi; Wala usiende na mtu wa ghadhabu nyingi; Usije ukajifunza njia zake; Na kujipatia nafsi yako mtego." (MITHALI 22:24-25).
Mtego huo hutoka kwa Shetani ili akuingize dhambini. Hivyo basi; matokeo ya hasira ni KUTENGWA NA WATU. Kwa kuwa mtu huyo hufanya maamuzi bila kutumia akili, hekima wala busara.
Neno la Mungu linapotuambia: "UCHUNGU WOTE NA GHADHABU NA HASIRA NA KELELE NA MATUKANO YAONDOKE KWENU, PAMOJA NA KILA NAMNA YA UBAYA.." Mungu anatutaka vitu hivyo viondoke kwetu kwa ajili ya faida yetu wenyewe. Lakini ukishindwa kuvidhibiti, matokeo yake utafikia hatua itakayokupa hasara kimwili na kiroho pia. Na ufahamu kwamba; MTU KUSHINDWA KUDHIBITI UCHUNGU USIMTAWALE kunaweza kuwa CHANZO CHA MABAYA NA DHAMBI KUTOKEA. Ndiyo maana utaweza kuona mtu amegombana na mke wake nyumbani alafu anaondoka na hasira zake kisha unasikia amegongwa na gari barabarani. Sasa jiulize, kusamehe ni kwa ajili ya faida kwa Mungu au kwako wewe mwenyewe? Au yawezekana umedhurumiwa pesa zako na wafanya biashara wenzako kisha ukaingia ofisini mwako umejaa hasira, wateja wanapokuja wewe unawajibu vibaya; Je, biashara yako ikifa utamlaumu Mungu, Shetani au lawama ni juu yako wewe uliyeshindwa KUZUIA HUO UCHUNGU? Dawa ya kuushinda uchungu ni KUSAMEHE; hakuna tiba nyingine zaidi ya KUSAME. Ni kitu cha kushangaza hata watu wadunia wanataka kuwazidi akili baadhi ya watu wa Mungu. Katika accountance kuna kitu kinaitwa Bad Debt Account. Yaani ni deni lililoshindikana kulipwa aidha kwa kudhurumiwa au mdeni amekufa au kufirisika. Wahasibu hufungua account hiyo ambayo ni ishara ya kusamehe deni lililoshindikana kulipwa, kisha wanafanya mikakati mipya ya kusawazisha pengo hilo. Sasa je! Kuna tatizo gani linalowafanya watu wa Mungu washindwe KUSAMEHE?
Nikifungua Biblia kwenye kitabu cha WAEFESO 4:26 Biblia inasema:
"Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na UCHUNGU wenu bado haujawatoka." (Efe 4:26)
Unaona sasa; tatizo kubwa la watu ni kuruhusu UCHUNGU KUWATAWALA. Tunapoambiwa "MWE NA HASIRA, ILA MSITENDE DHAMBI.." Kumbe inawezekana kabisa mtu kupatwa na hasira kwa sababu makwazo na majaribu ni mengi tuyapatayo kila siku, lakini tumeambiwa “MWE NA HASIRA LAKINI MSITENDE DHAMBI”;  na tena tunaambiwa “...JUA LISIZAME TUKIWA BADO NA UCHUNGU NDANI YETU.” Tunalazimika KUSAMEHE kwa ajili  ya faida yetu sisi wenyewe. Ndiyo maana tukisoma WAEFESO 4:26 imeandikwa: "wala msimpe Ibilisi nafasi."
 Hivyo basi, kumbe KUTAWALIWA NA UCHUNGU NI NJIA YA KUMPA SHETANI NAFASI. Tunaposoma WAEFESO 5:17 tunaona imeandikwa:
"Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana". (Efe 5:17)

Bila shaka hadi hapo nimeeleweka vizuri. Sasa basi;  Athali ya tatu ya KUTOKUSAMEHE ni kama ifuatavyo:

iii/: MUNGU HATAKUSAMEHE DHAMBI ZAKO.

KUTOSAMEHE ni moja ya sababu ya KUTOSAMEHEWA. Neno DHAMBI, lina maana ya kutenda kinyume na mapenzi ya Mungu. Dhambi ni kuvunja amri/sheria za Mungu. Mtu atendapo DHAMBI anakuwa haumkosei mwanadamu bali umemkosea Mungu. Hivyo basi, ni Mungu pekee ndiye awezaye KUKUSAMEHE. Kwa hiyo, Mungu hawezi kukusamehe wakati wewe hautaki KUSAMEHE wenzako.
 Neno la Mungu linatuambia kwamba:
"Nanyi, kila msimamapo na kusali, SAMEHENI, mkiwa na neno juu ya mtu; ILI NA BABA YENU ALIYE MBINGUNI AWASAMEHE NA NINYI MAKOSA YENU." (Marko 11:25)
Tukizidi pia kusoma ule mstari wa 26, tunaona Mungu anasisitiza kwa kusema:
"Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu." (Marko 11:26)
Mungu ametuweka wazi kabisa; ENDAPO KAMA SISI HATUSAMEHE, VIVYO HIVYO NA SISI HATUTASAMEHEWA. Sasa je! Ni nani asiyetenda makosa au kumkwaza mwenzake kwa namna yoyote ile? Bila shaka hapa jawabu ni HAKUNA. Kila mmoja wetu umkwaza mwenzake kwa namna fulani fulani. Kwa hiyo hatupaswi kuruhusu UCHUNGU ututawale hata kidogo ili Shetani asipate nafasi ndani yetu. Kwa kuwa sote huwa tunakoseana, ni lazima tusameheane ndipo na sisi tupate kusamehewa na Mungu.
Madhara mengine ya kutosamehe ni haya yafuatayo:
iv/: MUNGU HAPOKEI SADAKA ZAKO, NA WALA HAJIBU MAOMBI YAKO.
Nikifungua Biblia Takatifu kwenye kitabu cha MATHAYO 5:23,24 tunaona pameandikwa kwamba:
"Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako."
Mungu huchukizwa na sadaka za mwenye dhambi. Sadaka za mtu mwenye dhambi hazipokelewi mbele za Mungu. Ndiyo maana imeandikwa kuwa utii ni bora kuliko dhabihu. Mungu si masikini hata ababaishwe kwa sadaka zako. Tukisoma kitabu cha HOSEA 6:6 Mungu anasema:
"Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka...",
Mungu hababaishwi na hako kasadaka kako. Mungu si masikini hadi ababaishwe na uto tusadaka twako. Mungu anapenda sadaka za mtu mwenye moyo safi; Ndiyo maana Biblia inasema kwenye MITHALI 21:3
"Kutenda haki na hukumu humpendeza BWANA kuliko kutoa sadaka." (Mithali 21:3)
Mungu hupendezwa na moyo safi; ndiyo maana amesema "...IACHE SADAKA YAKO MBELE YA MADHABAHU, UENDE ZAKO, UPATANE KWANZA NA NDUGU YAKO, KISHA URUDI UITOE SADAKA YAKO." Kwahiyo, usipopatana (sameheana) na yule mliyekoseana, hakika Mungu hatapokea sadaka zako. Hivyo basi, KUTOSAMEHE umfanya mtu kukosa kibali mbele za Mungu. Naunapokosa kibali kwa Mungu maana yake unakuwa haujampendeza Mungu, vivyo hivyo kwa maana nyepesi unakuwa umetenda dhambi, kwa maana dhambi ni kutenda kinyume na mapenzi ya Mungu.
Hivyo basi, ninapenda kuhitimisha somo hili kama ifuatavyo; Biblia inasema kwenye kitabu cha WAEFESO 6:10,12
"Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani."
Ninajua wapo watu ambao watauliza; Je, silaha za Mungu ni zipi?
Silaha kubwa kabisa kuliko zote ni NENO LA MUNGU lililomo ndani ya Biblia Takatifu; neno hilo la Mungu linapaswa kukaa kwa wingi ndani yako. Neno la Mungu likikaa kwa wingi ndani yako, ukilifanyia kazi na kulishika, ndipo Roho Mtakatifu atakaa ndani yako na kukuongoza namna ya kufanya. Pasipo Neno la Mungu, hatuwezi kuyajua mapenzi ya Mungu. Kwahiyo, silaha kuu ni NENO LA MUNGU. Ndiyo maana tukisoma WAEFESO 6:14-17 imeandikwa:
"Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu..."
Sasa soma hapa kwa makini zaidi, "...Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu."
Siku zote Shetani anataka kuona watu wanapotea na kukosa baraka za Mungu. Shetani analeta majaribu na makwazo mbalimbali ili watu waanguke na kuiacha njia ya uzima; Shetani anataka watu wawe na uchungu ili wakose baraka za Mungu. Hauwezi kusema umemsamehe mtu wakati bado unao uchungu moyoni mwako. Biblia inasema hakuna dhambi ndogo wala dhambi kubwa, ni kwa sababu muongo na muuaji wote hukumu yao ni kutupwa kwenye ziwa la moto na kupata humo mateso ya milele yote. Vivyo hivyo yeye asiyesamehe wenzake hukumu yake ni ile ile kwenye ziwa la moto sawa sawa na muuaji.
Nikisoma WAEFESO 6:12 imeandikwa
"Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."
Ndugu zangu tuweni macho na makini sana, Shetani hapendi kuona watu wanabarikiwa, hapendi kuona kazi ya Mungu inasonga mbele, na hapendi kuona watu wanarithi uzima wa milele. SAMEHEANENI NA WALA UCHUNGU USIKAE MIOYONI MWENU. Mwenyezi Mungu awabariki nyote mnaotendea kazi haya mliyojifunza humu. Roho Mtakatifu awaongoze kwenye kweli yote, mbarikiwe katika jina la Yesu Kristo. Amina.

Comments

Popular Posts