DHAMBI ZOTE ZINASAMEHEKA MBELE ZA MUNGU KASORO MOJA TU....

DHAMBI ISIYO SAMEHEWA...! ! !

Bwana Yesu amesema kwamba: "...Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho Mtakatifu hawatasamehewa." - (Mathayo 12:31)

Je! Nini maana ya KUMKUFURU Roho Mtakatifu?
 Tukianza na neno KUFURU, maana yake ni: Kusema maneno yakumtukana Mungu au kufanya matendo yanayomtukana Mungu. Tukiendelea kusoma Mathayo 12:32 tunaona Bwana Yesu anasema kwamba:

"Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao." (Mathayo 12:32)

Ni kweli kuwa Yesu ni Mungu; lakini, Je! Yesu anamaanisha nini kuhusu dhambi isiyosamehewa ya KUMKUFURU Roho Mtakatifu?
Kumkufuru Roho Mtakatifu maana yake ni hii; Biblia Takatifu inasema kwamba:

"Kwa maana HAO WALIOKWISHA KUPEWA NURU, na KUKIONJA KIPAWA CHA MBINGUNI, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu, na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo, wakaanguka baada ya hayo, HAIWEZEKANI KUWAFANYA UPYA TENA HATA WAKITUBU; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na KUFEDHEHESHA kwa DHAHIRI." (Waebrania 6:4-6)

Kumkufuru Roho Mtakatifu ni kuzitukana kazi za Mungu ambazo hakika kazi hizo ziliwahi kuyagusa maisha yako. Hapa namaanisha ya kwamba: mf. Yawezekana mtu alikuwa ni Mkristo na analijua neno la Kristo vizuri; mtu huyo baadae akaja akakengeuka na kuanza kuutukana Ukristo pamoja na matendo ya Mungu ambayo yanatendeka kwa uwezo wa Roho Mtakatifu; mtu huyo atakuwa ANAMKUFURU Roho Mtakatifu na KAMWE HATASAMEHEWA.
Tumeona hapo Biblia Takatifu imesema kuwa: "...wakaanguka baada ya hayo, HAIWEZEKANI KUWAFANYA UPYA TENA HATA WAKITUBU..." (Ebr 6:6) ni kwa sababu wamefanya "...KUFEDHEHESHA kwa DHAHIRI." Wamezitukana kazi za Mungu kwa makusudi; dhambi hiyo ndiyo Yesu anasema kamwe haitasamehewa. Biblia Takatifu inazidi kusema kwamba:

"Maana, kama TUKIFANYA DHAMBI KUSUDI baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, HAITABAKI TENA DHABIHU KWA AJILI YA DHAMBI; bali kunakuitazama hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao. Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma... Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano ALIYOTAKASWA KWAYO kuwa ni kitu ovyo, na KUMFANYIA JEHURI Roho wa neema?" (Waebrania 10:26-29)

Kuzitukana kazi za Mungu ni dhambi ambayo kamwe haiwezi kusamehewa. Tunapaswa tuwe makini sana juu ya hili. Leo hii tumepewa neema ya wokovu; na pia tumeziona kazi za Mungu maishani mwetu; isije ikatokea siku mmoja wetu akakengeuka na kuutukana Ukristo. Hilo ni jambo la kutisha na KAMWE HALITASAMEHEWA.

Wapendwa; Tusonge mbele katika wokovu. Tuishi maisha ya toba kila wakati; na pia, tuzidi kuihubiri kweli ya neno la Mungu bila ya kujitakia maslahi binafsi.

"Ee Bwana Yesu, nakuomba uwe nasi daima; kamwe asije akatokea mmoja miongoni mwetu akazikufuru kazi Zako. Naomba Roho Mtakatifu uwe nasi daima; utuongoze na kutulinda katika jina la Yesu Kristo. Amina."

Comments

Popular Posts