IKIMBIENI ZINAA
SOMO: IKIMBIENI ZINAA
Wiki ya Kwanza
Je! Unaamini ya kuwa Mungu anaweza kusema na watu kwa njia ya
ndoto? Najua ni rahisi kuamini kuwa Mungu alisema na watu zamani kwa
njia ya ndoto kama tunavyosoma katika Biblia; lakini je! Unaamini ya
kuwa Mungu anasema na watu kwa njia ya ndoto siku hizi?
Najua kuna watu wanaoamini na wengine hawaamini. Sijui wewe
uko upande gani.
Lakini nataka nikueleze hivi; Kufuatana na Biblia kuna ndoto
za aina tatu;
(a) Kuna ndoto kutoka kwa Mungu. Soma kitabu cha Hesabu
12:6, na Yoeli 2:28.
(b) Kuna ndoto zinakuja kwa sababu ya shughuli nyingi. Soma
kitabu cha Mhubiri 5:3.
(c) Kuna ndoto za uongo zinazotoka kwa shetani aliye baba
wa uongo. Soma kitabu cha Yeremia 23:52 na Yohana 8:44.
Unaweza kutofautisha kwa namna gani tofauti iliyopo kati ya hizi ndoto?
Na utajuaje kuwa ndoto uliyoiota imetoka kwa Mungu? Kila ndoto lazima
ipimwe na Neno la Mungu. Ikiwa imetoka kwa Mungu, ni lazima utakuta neno
la Mungu ambalo linaeleza maana yake. Mara nyingine ndoto toka kwa
Mungu huja kama fumbo; lakini Roho Mtakatifu ajuaye kuyafumbua mafumbo
ya Mungu (1 Wakorintho 2:10,11), atalifunua fumbo hilo kwa kukuonyesha
neno la Mungu linalofanana na ndoto hiyo.
Si busara kuzikubali ndoto zote unazoota bila ya kuzipima katika Neno la
Mungu. Na pia si busara kuzikataa ndoto zote bila kuzipima katika Neno
la Mungu.
Nimeona nianze kwa kukueleza haya kwa kuwa chanzo cha kuandika kitabu
hiki, ni ujumbe wa Mungu ulionijia kwa njia ya ndoto.
Ndoto yenyewe ilikuwa hivi: Niliona katika ndoto mtu mmoja mkristo, tena
aliyeokoka akifanya mambo ya zinaa bila hata kuogopa. Na wakati
nilipokuwa nikimtazama na kusikitika, nikasikia sauti toka juu yangu
ikisema;
“ NITACHUKULIANA MPAKA LINI NA MWANADAMU AFANYAYE MAMBO YA JINSI HIYO?”
Baada ya kusikia maneno hayo nikaamka.
Wakati huo ulikuwa ni alfajiri, na ndoto hiyo ilinipa maswali na
masononeko mengi moyoni mwangu. Na niliamua kumshirikisha mke wangu
Diana juu ya ndoto hiyo.
Mke wangu akaniuliza; “ Maana yake nini ndoto hiyo?”
Nilipotaka kufungua kinywa ili nimjibu uchungu mzito ulijaa moyoni
mwangu, nikasikia kuugua rohoni, na mara nikaanza kulia!
Unaweza ukaniuliza; “Mwakasege kwa nini ndoto ikulize machozi?”
Hili ni swali zuri. Hata mimi nilijiuliza kwa nini nitoe machozi kwa
ajili ya ndoto. Lakini baada ya kulifuatilia jambo hili katika maombi na
katika neno la Mungu nilielewa sababu yake.
Je! Unafahamu matokeo ya Mungu kusema “Nitachukuliana mpaka lini na
mwanadamu afanyaye mambo ya jinsi hiyo?” Ukisikia maneno ya jinsi hii
ujue Mungu amekasirika na kuna maangamizo mbele.
Hebu na tulifuatilie jambo hili katika biblia ili tulione uzito wake.
Nuhu na Gharika.
Ni vizuri ukumbuke ya kuwa gharika ilitokea wakati wa Nuhu kwa sababu ya
zinaa.
“Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike
walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliona hao binti za wanadamu – ni
wazuri; WKAJITWALIA WAKE WO WOTE WALIOWACHAGUA. Bwana akasema, ROHO
YANGU HAITASHINDANA NA MWANADAMU MILELE, kwa kuwa yeye ni nyama; basi
siku zake zitakuwa mia na ishirini. Nao Wanefili walikuwako duniani
siku zile, tena baada ya hayo, wana wa Mungu WALIPOINGIA kwa binti za
wanadamu, wakazaa nao wana; hao ndio waliokuwa watu hodari zamani, watu
wenye sifa. BWANA AKAONA YA KUWA MAOVU YA MWANADAMU NI MAKUBWA DUNIANI
NA KWAMBA KILA KUSUDI ANALOWAZA MOYONI MWAKE NI BAYA TU SIKU ZOTE. BWANA
AKAGHAIRI KWA KUWA AMEMFANYA MWANADAMU DUNIANI, AKAHUZUNIKA MOYONI.
Bwana akasema, Nitamfutilia usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na
kitambulisho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba
nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Bwana.” (Mwanzo 6:1-8)
Ukiendelea kufuatilia habari hii katika Biblia utaona ya kuwa baada ya
gharika ya maji walibaki watu nane tu! Wanadamu wengine wote waliangamia
kwa sababu ya nini? – Zinaa!
Sodoma na Gomora
Wasomaji wa Biblia wanafahamu kabisa ya kuwa miji ya Sodoma na Gomora
iliteketezwa kwa moto baada ya Mungu kuihukumu kwa sababu ya uasherati
uliokuwa ukifanyika ndani yake. Soma Mwanzo 19:4-25.
Na pia katika kitabu cha Yuda 1:7 tunasoma hivi: -
“Kama vile Sodoma na Gomara, na miji iliyokuwa kando kando, waliofuata
UASHERATI kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo
ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa milele.”
Ikiwa Mungu aliwatenda hivi watu wa Sodoma na Gomora, ni kitu gani
kinamfanya mwanadamu wa siku hizi adhani ya kuwa Mungu amebadilika juu
ya kuadhibu wale wote wafanyao uasherati? Katika miji hiyo miwili ni
watu watatu tu waliobaki – Lutu na watoto wake wawili! Wanadamu wengine
waliokuwa katika miji hiyo waliteketezwa kwa sababu ya nini – Zinaa!
Kuhani Eli na watoto wake.
“Basi Eli alikuwa mzee sana, naye alisikia habari za mambo yote ambayo
wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi WALIVYOLALA NA WANAWAKE waliokuwa
wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania.” (1Samweli 2:22)
Hata baada ya baba yao kuwaonya hawakusikia, na matokeo yake ni:-
1. Watoto hao wawili, Hofni na Finehasi walikufa wote
siku moja;
2. Wana wa Israeli walipigwa na adui zao Wafilisti na
Sanduku la agano likatekwa;
3. Kuhani Eli alikufa.
Yote haya yalitokea katika taifa ambamo watoto wawili wa kiongozi
waliuwa wakifanya mambo ya Zinaa bila hata kujali maonyo.
Je! Bado unajiuliza kwa nini nilitoa machozi baada ya kusikia sauti ya
Mungu katika ndoto ikisema “Nitachukuliana mpaka lini na mwanadamu
afanyaye mambo ya jinsi hiyo?”
Siku za Mwisho.
“Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za
hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda
fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi
wao, wasio na shukrani, wasio safi…….Kwa maana katika hao wamo wale
WAJIINGIZAYO KATIKA NYUMBA ZA WATU, NA KUCHUKUA MATEKA WANAWAKE WAJINGA
WENYE MIZIGO YA DHAMBI, waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi. (2
Timotheo 3:1,26).
Je! Siku hizi wanawake hawatekwi mateka na wanaume ili wafanye mambo ya
zinaa? Vishawishi vimekuwa vingi, na wanawake wengi wameanguka katika
mitego hiyo ya kupenda fedha na anasa, na mwisho wake ni kufanya
uzinifu.
Kwa nini wanaume wengi wamekosa akili juu ya jambo hili. Ni kitu gani
kimewapofusha macho wasione ya kuwa uzinifu ni mbaya? Biblia inasema;
“Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; afanya jambo
litakalomangamiza nafsi yake.” (Mithali 6:32)
Ni dhahiri ya kwamba palipo na zinaa pana uharibufu, na wengi
wanaangamia. Na nataka nikuambie ya kuwa Roho Mtakatifu akikuwekea mzigo
huo ndani yako na kuliona jambo hili jinsi linavyomhunish Mungu, hakika
hutatulia; na hapana budi macho yako yatajaa machozi juu ya kizazi hiki
kinachojiangamiza chenyewe kwa sababu ya zinaa.
Sababu ya mambo haya kuandikwa.
Mambo haya hayakuandikwa kwa bahati mbaya, wala si kwa ajili ya
kuonyesha historia ya watu Fulani tu. Bali yaliandikwa kwa kusudi
maalumu na muhimu.
“Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili
KUTUONYA SISI, tuliofikiriwa na miisho ya zamnai – Kwa hiyo
anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.” (1 Wakorintho
10:11,12)
Na mimi nimependa kuyaonyesha wazi ili tujue tunapozungumza juu ya
zinaa, Bwana Mungu anakuwa na mawazo gani juu yake. Nafahamu si mara kwa
mara hata katika mahubiri na mafundisho, jambo hili huguswa kwa undani.
Lakini naona umefika muda wa kulichambua jambo hili kwa undani zaidi.
Hali ilivyo sasa.
Mtu mmoja aliniuliza “Je, mtu aliyeokoka anaweza kufanya mambo
ya uasherati – je, anaweza kuzini?”
Nikamwambia, “Mtu aliyeokoka hatakiwi kufanya mambo ya
uasherati, kwa kuwa kufanya hivyo ni dhambi, lakini asiposimama katika
Kristo sawasawa anaweza kuzini.”
Halafu huyo mtu akaendelea kuuliza, “Je, Unamfahamu Fulani?
(Akamtaja jina lake).
“Ndiyo namfahamu.” Mimi nilimjibu, na nikaendelea kusema; - “
kuwa ni mtumishi wa Mungu, ingawa sijamwona muda mrefu umepita sasa”.
Ndipo akasema, “Unafahamu ya kuwa alianguka na akazini na
msichana Fulani (akamtaja jina lake) ambaye pia ameokoka, na sasa yule
msichana amezaa?”
Mimi nilishangaa na kushutushwa na habari hizo. Nikamuuliza
“Unasema kweli ndivyo ilivyotokea?”
Akasema, “Ndiyo”
Ndipo Roho wa Mungu aliponikumbusha ndoto ile aliyonipa.
Katika ujumbe ule wa ndoto, Mungu alinionyesha mkristo aliyeokoka
akifanya mambo ya uasherati.
Kwa mtu asiyeokoka siwezi kushangaa akifanya uzinzi, kwa kuwa
bado yuko gizani, na yuko chini ya mkuu wa giza, ibilisi – kwa hiyo
anaweza kufanya lo lote lile. Ndiyo maana mtu anaweza kusema yeye ni
mkristo, na huku anazini mara kwa mara.
Mkristo wa kweli aliyeokoka hatakiwi kuzini, wala kushindwa na
dhambi. Kwa nini? Kwa kuwa ndani yake ametengwa mbali na dhambi, na
amepewa ushindi juu ya dhambi.
Ushindi dhidi ya dhambi
Uhusiano wako na dhambi unakuwaje baada ya kuokoka, na
kufanyika kiumbe kipya ndani ya Kristo? Watu wengi wakiisha-okoka, huwa
bado wanasumbuliwa na kuanguka katika dhambi mara kwa mara, na hasa
katika zinaa. Na hii inatokea kwa kuwa hawapati mafundisho ya kutosha ya
neno la Mungu juu ya jinsi wanavyotakiwa kuenenda katika maisha mapya
waliyopita.
Kaini aliambiwaje na Mungu? Bwana alimwambia hivi; “ kama
ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea
mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa UISHINDE” (Mwanzo 4:7)
Na ndivyo ilivyo hata sasa. Bado tumo ulimwenguni humu, ingawa
aliyezaliwa mara ya pili yeye si wa ulimwengu huu (Yohana 17:16).
Lakini kwa kuwa bado tumo katika ulimwengu uliojaa dhambi inayotutamani
kila siku, na tusije tukajisahau. Inatupasa tuishinde.
Yanenaje maandiko?
Imeandikwa katika kitabu cha (Warumi 6:12-14)
“Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na mauti, hata
mkazitii tamaa zake; wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za
dhuluma kwa dhambi, bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada
ya kufa, na viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi, bali
jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu
kwa Mungu kuwa silaha za haki. Kwa maana DHAMBI HAITA WATAWALA NINYI,
kwa sababu hamuwi chini ya sheria, bali chini ya neema”.
Ikiwa tunaambiwa ya kuwa “Dhambi haitawala ninyi …….” inakuwaje basi
wengine wanatawaliwa nayo? Inakuwaje mtu wa Mungu, aliyepakwa mafuta kwa
Roho Mtakatifu aanguke katika zinaa? Kitu gani kinampofusha macho ya
rohoni?
Je! Ni halali kwa mtu anayekaa ndani ya Kristo kutenda dhambi?
Yanenaje maandiko?
“Kila akaaye ndani yake (Yesu Kristo) HATENDI DHAMBI; kila atendaye
dhambi hakumwona yeye, wala hakumtamua….atendaye dhambi ni wa ibilisi;
kwa kuwa ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa
Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.” (1 Yohana 3:6,8)
Je! Unaona maneno haya yalivyoandikwa kwa ajili yetu? Sidhani kama
unapenda tena kuwa Ibilisi kwa kuwa “Apendaye dhambi ni wa Ibilisi” Kwa
hiyo ni muhimu ujilinde usitende dhambi.
Tena imeandikwa:
“Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu UZAO WAKE
WAKAA NDANI YAKE; WALA HAWEZI KUTENDA DHAMBI KWA SABABU AMEZALIWA
KUTOKANA NA MUNGU.” (1 Yohana 3:9)
Ikiwa umezaliwa mara ya pili kwa Roho wa Mungu, ujue hakika UZAO WA
MUNGU unakaa ndani yako. Na uzao huu wa uungu ni Mtakatifu, na unakaa
ndani yake bila kutangatanga unakuwezesha kuishi bila kutenda dhambi.
Je! Si jambo la kumshukuru Mungu hilo. Si kwamba anatuambia tusitende
dhambi bila kutupa njia ya kutusaidia. Anajua sisi wenyewe hatuwezi
kuishinda dhambi, BALI YEYE AKIKAA NDANI YETU NA SISI NDANI YAKE
TUNAWEZA KUISHI KATIKA USHINDI DHIDI YA DHAMBI NA MITEGO YAKE YOTE.
Tena imeandikwa;
“Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu HATENDI DHAMBI; bali yeye
aliyezaliwa na Mungu HUJILINDA, wala yule mwovu HAMGUSI.” (1 Yohana
5:18)
Ee, mtu wa Mungu, jilinde basi kwa kuwa umezaliwa na Mungu, kwa nini
tamaa ya uasherati ikusonge? Je?! umesahau ni uzao wa namna gani ulio
ndani yako?
Ni kweli kwamba mtu akitenda dhambi na akatubu, Bwana atamsamehe, (1
Yohana 1:9). Lakini hatutakiwi kutenda dhambi. Ndiyo maana imeandika;
“Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba MSITENDE DHAMBI”…. (1
Yohana 2:1)
Sasa naona unaweza kuelewa kwa nini inashtusha na kusikitisha unaposikia
mtu wa Mungu ameanguka katika dhambi ya zinaa. Ikiwa maisha ya wokovu
yatakuwa ni ya kuanguka na kusimama, halafu tena kuanguka na kusimama
mara kwa mara; basi ina maana ya kuwa ushindi wa kutosha haukupatikana
pale msalabani.
Lakini nataka nikuambie hivi, ushindi kamili ulipatikana pale msalabani
bila kubakiza kitu! Ndiyo sababu Yesu Kristo alikuwa na ujasiri wa
kusema ‘IMEKWISHA’ pale msalabani.
Tunachotakiwa kufanya ni kuwa watendaji wa neno; na ndiyo ushindi huo
utadhihirika katika maisha yetu. Usidhani ya kuwa mapokeo ya wanadamu
yanaweza kukusaidia kuishinda dhambi; la hasha! Yesu Kristo peke yake
akikaa ndani ya moyo wako, na neno lake ukilitii, ndiko utapata
ushindi halisi na halali dhidi ya dhambi.
Swali la kujiuliza
Idadi ya wakristo waliookoka wanaoanguka katika dhambi ya zinaa
inaongezeka siku baada ya siku. Na wengine wameanguka dhambini moja kwa
moja, hata haja ya kutaka kusimama upya katika Bwana imepotea. Wanaona
aibu! Na wengine wanaanguka na kusimama, halafu tena wanaanguka na
kusimama. Na kwa sababu hiyo hawana ushuhuda mzuri mbele za watu.
Hawaaminiki tena.
Lakini je! Unadhani Mungu atatuambia tuishinde dhambi wakati anafahamu
ya kuwa hatuna uwezo huo? La hasha! Mungu wetu tunayemwamini katika
Kristo Yesu si dhalimu kiasi hicho.
Jambo ninalofahamu ni kwamba ametuambia tuishinde dhambi kwa kuwa ndani
yetu sisi tuliompokea, ametupa UWEZA WA KUISHINDA DHAMBI – kwa namna
gani?
“Kwa sababu UZAO WAKE WAKAA NDANI YAKE (YETU) WALA HAWEZI (HATUWEZI)
KUTENDA DHAMBI KWA SABABU AMEZALIWA (TUMEZALIWA) KUTOKANA NA
MUNGU”.(1Yohana 3:9)
Uzao wako si uzao wa kuanguka dhambini, bali ni uzao wa kushinda dhambi,
kwa kuwa Kristo anakaa ndani yako!
Ikimbieni Zinaa / 1 / 2 / 3 / 4 /
IKIMBIENI ZINAA
SOMO: IKIMBIENI ZINAA
Wiki ya Pili
MKRISTO ANAANGUKAJE KATIKA ZINAA?
Kila mara nilipopata habari za watu wa Mungu walioanguka
katika dhambi ya zinaa nilikuwa najikuta najiuliza swali hili, “Hivi
wanapataje ujasiri wa kutenda tendo hilo?”
Akili yangu ilikuwa inakataa kabisa kuamini kuwa mtu
aliyeokoka (na wakati mwingine amejazwa Roho Mtakatifu) anaweza kuanguka
kwenye dhambi ya zinaa. Lakini hata hivyo bado nikawa naendelea kusikia
majina ninayoyafahamu ya watu wa Mungu waliookoka waliokubwa na dhambi
ya zinaa.
“Wanafanyaje mpaka wanaanguka katika zinaa”? Hili swali lilinisumbua kwa
muda mrefu. Na siku moja nilikuwa nyumbani kwangu nikijiuliza swali
hili moyoni, nikasikia Roho Mtakatifu akiniuliza ndani ya moyo wangu,
akisema, “ Kwani Daudi aliangukaje? Je! Umesahau ya kuwa naye alikuwa
mtu wangu, mtumishi wangu niliyempaka mafuta?
Niliposikia swali hili, nilichukua biblia na kusoma maneno
yanayoeleza kuanguka kwa Mfalme Daudi katika dhambi ya zinaa na mke wa
mmoja wa askari wake.
Mambo niliyoyasoma yalinifungua macho kuona jinsi ambavyo hata
hivi leo watu wa Mungu wanavyoanguka au wanavyoweza kuanguka katika
dhambi ya zinaa.
Chukua biblia yako na usome habari hizi katika 2 Samweli
11:1-27 na 2 Samweli 12:1-25.
Chanzo cha kuanguka kwa Mfalme Daudi katika dhambi ya Zinaa,
ni KUTOKWENDA VITANI PAMOJA NA ASKARI WAKE.
“Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda
vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na
Israeli wote, wakaangamiza wana wa Amoni, wakakuhusuru Raba. LAKINI
DAUDI MWENYEWE AKAKAA YERUSALEMU”. (2 Samweli 11:1)
Kama kiongozi wao, Daudi alitakiwa kuongozana na watu wake
vitani, lakini yeye aliamua kubaki Yerusalemu asiende vitani, na
akamtuma mtu mwingine amwakilishe. Na jambo hili lilimpa nafasi nzuri
sana ibilisi ya kumpa Daudi kazi nyingine ya kufanya. Ni kazi gani hiyo?
“Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, AKATEMBEA JUU YA DARI
ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke ANAOGA;
naye huyo mwanamke alikuwa MZURI SANA WA KUPENDEZA MACHO”. (2 Samweli
11:2)
Ni kitu gani kilimfanya Mfalme Daudi aamue kutembea juu ya dari ya jumba
lake badala ya kwenda vitani pamoja na watu wake? Na alipomwaona
Bathsbeba, mkewe Uria akioga alishindwa kujizuia, mwisho wake ni kuzini
naye na huyo mama kupata mimba!
Wakristo wengi wamejikuta wameingia katika mtego wa zinaa kwa sababu ya
kutokwenda ‘Vitani’ wakati wanapotakiwa kufanya hivyo. Vita
tunavyovisema, si vita vya kimwili.
“Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya
mwili, maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika
Mungu hata kuangusha ngome; tukiangusha mawazo na kila kitu
kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila
fikra ipate kumtii Kristo”. (2 Wakorintho 10:3,4)
Na pia imeandikwa; “ Kwa maana kushindani kwetu sisi si juu ya damu na
nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili juu ya
majeshi ya pepo wabaya, katika ulimwengu wa roho”. (Waefeso 6:11)
Ndiyo maana Yesu Kristo alisema; “ Kesheni mwombe msije mkaingia
majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.” (Mathayo 26:41)
Usipovipiga vita katika maombi, inakuwa ni rahisi sana kuangushwa na
majaribu unapokutana nayo. Wakristo wakipoa katika maombi inakuwa rahisi
kuanguka katika dhambi, si katika zinaa peke yake, bali katika mtego
wowote ambao shetani anauweka mbele yao!
Kutokuwa mwombaji, ni sawa na kutokwenda vitani na wenzako, kama vile
Mfalme Daudi alivyofanya.
Kwa hiyo unaona ya kuwa ingawa Mfalme Daudi alikuwa mtu wa Mungu,
mtumishi wake, na mpakwa mafuta wake, alianguka katika zinaa. Na hata
hivi leo kuna wakristo, tena wameokoka, na kupakwa mafuta kwa Roho
Mtakatifu, wanaonguka katika dhambi ya zinaa. Kwa nini? Kwa kuwa
hawavipigi vita vya kiroho na wenzao, na wamepoa katika kumtumikia
Bwana.
Je! Lutu aliangukaje?
Hili ni swali ambalo Roho Mtakatifu aliniuliza baada ya kunieleza habari
za Mfalme Daudi. Ingawa Lutu alikuwa mtu wa Mungu, na licha ya kuwa
alikuwa anabebwa kwa maombi ya Ndugu yake Ibrahimu, bado alianguka
katika zinaa.
Roho Mtakatifu alikuwa anaendelea kunijibu swali nililokuwa najiuliza ya
kuwa, watu waliookoka wanaangukaje katika zinaa?
Habari za kuanguka kwa Lutu zimeandikwa katika kitabu cha Mwanzo
19:30-38.
Lutu alizini na watoto wake wawili wa kike baada ya kuleweshwa mvinyo.
Na ukiisoma habari hii inasikitisha sana. Shetani alipata nafasi ya
kumwangusha Lutu si kwa sababu ya binti zake kumlewesha mvinyo, bali kwa
kuwa MKE WAKE HAKUWA PAMOJA NAYE. Unadhani mke wake angekuwapo hawa
watoto wangepata nafasi ya kumlaghai baba yao? Hapana! Kwa nini?
Kwa maana “ Bwana ameumba jambo jipya duniani, mwanamke atamlinda
mwanaume.” (Yeremia 31:22)
Unaweza kujiuliza ni kwa njia gani mke atalimnda mume wake. Kumbuka
imeandikwa mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana. Kazi moja ya busara
iliyo ndani ya mke ni kumlinda mume kutokana na mashambulizi ya Malaya!
Soma Mithali 2:11-22.
Hata hivi leo ndoa ambazo mume na mke hawakai vizuri, huwa ni rahisi kwa
wao kuanguka katika dhambi ya zinaa hata kama wameokoka. Na huu siyo
ushuhuda mzuri.
Tunamshukuru Mungu kwa wale ambao wamesimama katika ushuhuda ingawa ndoa
zao zina matatizo.
Jambo la kujifunza zaidi
Roho Mtakatifu alipokuwa anaendelea kunifundisha akasema ndani ya moyo
wangu hivi; “Watu wengi wanadhani zinaa ni tendo la kimwili tu
linalofanywa kati ya mwanaume na mwanamke nje ya ndoa, lakinikuna namna
zaidi ya moja unayoweza kuanguka katika zinaa.”
Niliposikia hivyo moyoni mwangu, niliichukua biblia na nikaanza kuisoma
upya juu ya zinaa na nikaona kuna namna nne ambazo zinaa inatajwa:-
1. KATIKA MWILI:
“….Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa
mwili. Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae
viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya Kahaba? Hasha! Au hamjui ya
kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? …. Ikimbieni zinaa,
kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye
zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa mwili
wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu?
Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa
basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.” (1 Wakorintho 6:13-20)
2. KUTAMANI KWA MACHO. Yesu Kristo alisema;
“Mmesikia kwamba imenenwa Usizini; lakini mimi nawaambia, kila mtu
AMTAZAMAYE MWANAMKE KWA KUMTAMANI, amekwisha KUZINI NAYE MOYONI MWAKE.”
(Mathayo 5:27,28)
3. KUACHA MKE NA KUOA MWINGINE
Yesu Kristo alisema;
“Kila amwachaye mkewe na kuoa mke mwingine azini ……” (Luka 16:18)
4. KUOA ALIYEACHWA. Yesu Kristo alisema;
“Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; NAYE AMWOAYE YEYE
ALIYEACHWA NA MUMEWE AZINI.” (Luka 16:18)
Kila mtu na ajipime katika hayo; ikiwa umefanya mambo kama
hayo niliyoyataja, biblia inasema UMEZINI! Je Hakuna waliokoka
wanaofanya mambo ya jinsi hii? Wanaowaacha wake zao halali? – Wanaooa
walioachwa? – na wanaozini katika mwili?
Ikimbieni Zinaa / 1 / 2 / 3 / 4 /
IKIMBIENI ZINAA
SOMO: IKIMBIENI ZINAA
Wiki ya Tatu
USHAURI WA BIBLIA JUU YA KUEPUKANA NA ZINAA
“Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa…..” (Hosea 4:6). Haya ni
maneno ambayo Bwana aliyanena kwa kutumia kinywa cha Nabii Hosea kwa
watu wake, wana wa Israeli. Lakini maneno haya yanatuhusu watu wake hata
leo.
Watu wa Mungu wengi sana nyakati hizi wanaangamizwa kwa kukosa maarifa –
maarifa juu ya mapenzi ya Mungu. Na eneo mojawapo ambalo linaangamiza
wengi ni eneo la uzinzi.
Kwa kukosa mafundisho ya kutosha juu ya neno la Mungu juu ya kusimama
katika Kristo na kuepukana na zinaa, watu wa Mungu wengi wameanguka
kiroho. Na wengine wanaishi maisha ya kuanguka na kusimama kuanguka na
kusimama, - kitu gani kinawaangusha – zinaa!
Ndiyo maana Nabii Hosea alitumiwa na Bwana kuendelea kusema kuwa;
“UZINZI na divai mpya huondoa FAHAMU za wanadamu” (Hosea 4:11). Kukosa
fahamu ni sawa na kutojitambua uko wapi na unafanya nini. Na hii ni
kweli kabisa, watu wanaofanya uzinzi wangekuwa na fahamu wangetubu na
kuacha upesi, kwani madhara yake ni makubwa.
Imeandikwa,
“Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo
litakalomwangamiza nafsi yake.” (Mithali 6:23)
Kukosa kujua neno la Mungu linasema nini juu ya zinaa katika marefu na
mapana yake, kumewafanya watu wengi wanaswe na mtego huu mbaya.
Kuna wakati fulani tukiwa kwenye mkutano wa kiroho mji mmoja hapa
nchini, aliokoka msichana ambaye alikuwa kahaba katika hotel moja. Na
wakati huo alipookoka alijazwa Roho Mtakatifu, akazungumza kwa lugha
mpya.
Baada ya wiki kama moja hivi, watu wengine waliokoka waliamua
kumtembelea, lakini hali waliomkuta nayo iliwasikitisha. Kwani walimkuta
amerudi nyuma kiroho na amerudi kwenye maisha yake ya zamani ya
ukahaba.
Alipoulizwa ni kwa nini imekuwa hivyo alijibu “ Naona nilikuwa
nadanganywa na mambo ya wokovu, ili niache maisha haya mzuri (ya
ukahaba)”
Je! Umeamini ya kuwa uzinzi huondoa fahamu za mwanadamu? Huyu binti
atasemaje maisha ya ukahaba ni mazuri kuliko maisha ya wokovu? Ni wazi
kwamba fahamu zake zimeondoka. Anafanya jambo la kumwangamiza nafsi
yake, na anasema hayo ndiyo maisha mazuri!
Lakini naamini kabisa ya kuwa binti huyu angepewa ushauri wa biblia juu
ya tatizo la zinaa, angekuwa na nafasi nzuri ya kuishi maisha ya ushindi
katika Kristo. Kwa kukosa mafundisho hayo muhimu, kulisababisha hasara
kwa nafsi yake.
Mambo matano muhimu ninayokwenda kuyajadili katika sura hii, ni ushauri
mzuri wa biblia utakaoweza kukusaidia kuishinda dhambi hii ya zinaa.
Lakini unabidi uwe mtendaji wa neno. Kuyasoma haya bila kuyatenda
hayatakusaidia. Bali ukiyatenda, hakika utauona mkono wa Mungu.
1. DUMU KATIKA MAOMBI
Yesu pale Gethsemane alisema;
“Je! Hamkuweza kukesha pamojanami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije
mkaingia majaribuni; roho i radhi. Lakini mwili ni dhaifu” (Mathayo
26:40-41)
Ukisha mpokea Kristo moyoni mwako, roho yako inakuwa radhi kumtii Kristo
na kutokutenda dhambi; lakini kumbuka kuwa roho yako bado imo katika
mwili ulio dhaifu ambao unataka kutenda dhambi.
Yesu Kristo alipokuwa akifundisha kuomba alisema sehemu mojawapo ya
maombi yetu iwe;
“Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu, Kwa kuwa ufalme
ni wako, na nguvu na utukufu, hata milele, Amina.” (Mathayo 6:13). Watu
wengine huwa wanaisema sala hii kikasuku bila kuangalia uzito wa maneno
yaliyomo. Lakini ukijua uzito wake hutachoka kuomba kwa “ Na usitutie
majaribuni.” Jaribu mojawapo ambalo unapaswa uombe uepushwe nalo ni
zinaa.
Wengine wakianguka katika zinaa, utawasikia wakijitetea na kusema;
“Nilibanwa mno hata nikashindwa kujizuia – nikaanguka katika zinaa.”
Unaweza ukajitetea hivyo, lakini ungeamua kushinda, Bwana angeuwezesha
kushinda. Kwa kuwa imeandikwa; “ Ninyi watoto wadogo mwatokana na Mung;
nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye NDANI YENU NI MKUU KULIKO aliye
katika dunia.” (1 Yohana 4:4) “ Lakini katika mambo hayo yote
TUNASHINDA NA ZAIDI YA KUSHINDANA kwa yeye (Yesu Kristo) aliyetupenda
(Warumi 8:73)
Na ni budi pia ukumbuke, kila jaribu lina njia ya kutokea, si katika
njia ya kushindwa bali katika mlango wa ushindi.
“Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke. Jaribu
halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu, ila Mungu ni
mwaminifu, ambaye HATAWAACHA MJARIBIWE KUPITA MWEZAVYO; lakini pamoja na
lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.” (1
Wakorintho 10:12-13)
Je! Hili si jambo zuri kufahamu ya kuwa Mungu wetu tunayemwabudu na
kumtumikia katika Kristo ni MWAMINIFU? Hili ni zuri sana! Kwa kuwa
hatatuacha tujaribiwe kupita tuwezavyo, lakini pamoja na lile jaribu
atafanya na mlango wa kutokea, ili tuweze kufanya nini? Ili tuweze
KUSTAHIMILI! Jina la Bwana libarikiwe daima!
Tafsiri nyingine inasema “Anayedhani amesimama imara ajihadhari
asianguke. Majaribu mliyokwisha pata ni kawaida kwa binadamu. Mungu ni
mwaminifu. Naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na
majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo
salama.”
2. DUMU KATIKA NENO LA KRISTO
Ili tuweze kuenenda katika upya wa maisha ndani ya Kristo tuliyempokea
mioyoni, tunahitaji kulijua na kulitenda Neno lake.
Tukilikosa neno lake, tutajikuta kila mara tunafanya mambo ya zamani
tuliyoyafanya tulipokuwa katika dhambi, ambayo hatupaswi kuyafanya sasa
tukiwa ndani ya Kristo. Hii ni kwa kuwa tumekuwa viumbe vipya!
“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale
yamepita; tazama yamekuwa mapya.” (2 Wakorintho 5:17)
Ni kweli umekuwa kiumbe kipya ukiwa NDANI ya Kristo, tamaa ya uzinzi
imehama! Ndiyo maana Yesu Kristo aliomba hivi; “Uwatakase kwa ile kweli,
neno lako ndiyo kweli”. (Yohana 17:17)
Tunahitaji utakaso wa Neno kila wakati kwa sababu zifuatazo:-
(a) Ili tusije tukatenda dhambi tena (Zaburi 119:9,11)
(b) Ili lituongoze tusije tukapita gizani, kwa kuwa Neno ni taa (Zaburi
119:105)
(c) Ili lituwezeshe kumtambua mtu mwenye mawazo mabaya ya dhambi
anapoongea na sisi. (Waebrania 4:12,13)
(d) Ili litulinde tusije tukaanguka katika mikono ya Malaya (Mithali
2:1-3,11, 16; Mithali 5:1-23; Mithali 6:20-35; Mithali 7:1-27, Mithali
23:26-28 na Mithali 30:18-20)
Naamini kabisa ya kuwa wakristo wakipata mafundisho ya kutosha ya neno
la Mungu maanguko katika dhambi tunayoyasikia sasa hatutayasikia. Kwa
kuwa watajifunza kuishi katika ushindi ule ambao Kristo alitushindia
pale msalabani.
Lakini inasikitisha kuona ya kuwa masomo ya neno la Mungu ya
kuwasimamisha wakristo kiroho hayafundishwi vya kutosha. Na hata yale
yanayofundishwa yanafundishwa juu juu tu. Na tuungane pamoja basi katika
kumwomba Bwana ainue walimu wengu katika Kanisa, na kwamba awape
ujasiri na muda wa kutosha wa kufundisha kile alichowapa kufundisha.
3. IKIMBIE ZINAA.
“IKIMBIENI ZINAA. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake;
ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.” (1
Wakorintho 6:18)
Ni kweli ya kwamba, biblia inasema “Basi mtiini Mungu. Mpingeni shetani,
naye atawakimbia.” (Yakobo 4:7). Lakini biblia haisemi ipingeni zinaa,
bali inasema IKIMBIENI ZINAA!
Watu wengi wameanguka katika zinaa, kwa kuwa wanajaribu kupingana nayo.
Mwisho wake wanazidiwa na wanazini. Kwa nini hawafuati ushauri huu wa
biblia unaosema ikiembieni zinaa?
Katika kitabu cha Mwanzo 39:6-12 tunasoma habari za Yusufu jinsi
alivyokabiliwa na jaribu la uzinzi, na jinsi alivyopona kwa kukimbia!
Hebu na tuisome habari hii:
“Naye Yusufu alikuwa mtu mzuri, na mwenye uso mzuri. Ikiwa baada ya
mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, LALA NAMI.
Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui
kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia
mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala
hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyaje
ubaya huu mkubwa nikamkosee Mungu? Akawa akizidi kusema na Yusufu siku
baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala aongee naye. Ikawa,
siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu
katika watu wa nyumbani humo ndani; huyo mwanamke akamshika nguo zake,
akisema, lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake. AKAKIMBIA.
Akatoka nje.”
Matokeo ya Yusufu kuikimbia zinaa ni KUFUKUZWA KAZI NA KUFUNGWA JELA.
Yusufu aliuliza; “Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?” Kwa kuwa
hakutaka kumkosea Mungu kwa kukubali kuzini, aliamua kukimbia bila
kujali kitu kitakachotokea baadaye.
Tunapata ushauri gani katika jambo hili?
Hebu soma haya kwa makini. Ni afadhali ufukuzwe kazi kuliko ukamkosea
Mungu kwa kuzini na mwenye nyumba aliyekuajiri!
Ni afadhali ufungwe kuliko ukamkosea Mungu kwa kuzini na hakimu au
askari polisi.
Ni afadhali utengwe kanisani, kuliko ukamkosea Mungu kwa kuzini na
mchungaji au na kiongozi ye yote wa kanisa!
Ni afadhali ufukuzwe kwa ndugu yako, kuliko ukamkosea Mungu kwa kukubali
kuzini naye!
Je! Unasikia ushauri huu wa Roho Mtakatifu anaotufundisha katika neno la
Mungu? Je, umesikia?
Usikubaliane na zinaa; wala usipingane nayo; bali IKIMBIE ZINAA!
4. Usimpe nafasi Ibilisi:
“…..wala usimpe Ibilisi nafasi” (Waefeso 4:27)
Biblia isingesema tusimpe Ibilisi nafasi kama tusingekuwa na uwezo wa
kumpa au kutompa nafasi katika maisha yetu. Mara nyingi Ibilisi anapata
nafasi ya kuingia katika maisha ya mkristo si kwa sababu amemwonea bali
ni kwa sababu amepewa nafasi.
Ni kweli kwamba kuna watu wanaoonewa na Ibilisi. Lakini kwa mtu
aliyezaliwa mara ya pili kwa Roho wa Mungu, amepewa mamlaka juu ya nguvu
zote za Ibilisi, wala hakuna kitu kitakachomdhuru. Soma Luka 10:19.
Ndiyo maana imeandikwa “…..wala msimpe Ibilisi nafasi.”
Mambo gani yanaweza kumpa nafasi Ibilisi katika maisha yetu, hata
atuangushe katika zinaa? Baadhi ya mambo hayo yanaeleza hapa:-
(a) HASIRA
Jambo mojawapo linalompa nafasi Ibilisi kuwaangusha watu katika zinaa ni
hasira iliyojaa uchungu.
“Mwe na hasira, ila msitende dhambi, jua lisichwe na uchungu wenu bado
haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi.” (Waefeso 4:26-27)
Kuna wakati Fulani nilimuliza msichana mmoja sababu zilizomfanya azae
kabla ya kuolewa; alinijibu hivi, “Wazazi wangu walinigombeza siku moja
na kunisingizia kuwa nafanya umalaya, na huku nilikuwa sifanyi. Na kwa
kusingiziwa hivyo pamoja na matusi niliyotukanwa nilibanwa na hasira. Na
nikaamua kuanza kufanya umalaya kwa kuwa sikuona uhalali kusingiziwa
kitu ambacho nilikuwa sifanyi, kwa hiyo nikaone heri nifanye ili
nikisemwa; nisemwe juu ya kitu ninachofanya kweli. Na matokeo yake ni
kupata mamba na kuzaa kabla ya kuolewa.”
Hali ya msichana huyu inawapata wengi. Na hata katika ndoa, chanzo
kikubwa cha mume au mke kutokuwa waaminifu katika unyumba wao ni chuki
na hasira iliyo kati yao. Mwingine anazini ili amkomoe mwenzake! Ole!
Hasira siyo tiketi yako ya kukufanya uzini.
“Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke
kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya, tena iweni wafadhili ninyi kwa
ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo
alivyowasamehe ninyi.” (Waefeso 4:31,32)
Ikiwa hasira inakusumbua, badala ya kumkosea Mungu kwa kuzini, jifunze
kusemehe na kusahau kwa kutumia uwezo wa Kristo aliye ndani yako.
(b) MAWAZO
Mtu mmoja alikuja kwangu na kuniomba nimwombee apone ugonjwa uliokuwa
unamsumbua.
Nikamuuliza; “ Ugonjwa huu ulikuanzaje?”
Akasema; “Wakati Fulani nilianguka katika zinaa, na baada ya hapo
nikaanza kuumwa ugonjwa huu.”
Nikamuuliza tena; “Je! Ulitubu baada ya kuzini? Akasema; “Ndiyo
nilitubu, hata nikawaomba watu waniombee nipone; wakaomba lakini
sikupona.”
Nikamjibu nikasema; “Lakini naona wewe ndiye mwenye shida – hukutubu
sawa sawa.
Kwa kuwa imeandikwa; “ Nanyi mtamtumikia Bwana, Mungu wenu naye
atakibarikia chakula chako, na maji yako; NAMI NITAKUONDOLEA UGONJWA
KATI YAKO.” (Kutoka 23:25)
Akasema; “ Ni kweli nimetubu na wala sijarudi tena kuzini, ila
kinachonisumbua ni mawazo. Kila wakati nakuta nawaza juu ya yule
mwanamke niliyezini naye, lakini kila ninapotaka kwenda kwake najizuia.”
Nikamwambia; “Je hujui ya kuwa unapomwazia mwanamke moyoni mwako kwa
kumtamani unazini naye? Na kwa ajili hiyo unahitaji kutubu upya, na
usimwazie tena kwa kumtamani.”
Watu wengi wanasumbuliwa na mawazo ya zinaa kama mtu huyu. Na wakati
mwingine wanajitahidi wasiwaze lakini wanashindwa. Na wengi wa wale
waliofanya zinaa kwa mwili huwa mara nyingi wamekwisha kuzini moyoni.
Usiwaze mawazo mabaya ya uzinzi, na kumpa nafasi Ibilisi! Jaza moyo wako
neno la Mungu, na utawaza neno la Mungu. Je hukumbuki kuwa imeandikwa
ya kuwa;
“Hatimaye, ndugu zangu, mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya
staha, yoyote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye
kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa
nzuri yo yote, YATAFAKARINI HAYO” (Wafilipi 4:8)
(c) MAENEO YASIYOFAA
Enyi wavulana jihadharini na ndugu zenu wa kike, na enyi wasichana
jihadharini na ndugu zenu wa kiume. Soma katika 2 Samweli 13:1-39 uone
jinsi mtu na dada yake walivyoanguka katika zinaa. Tafadhali uwe
mwangalifu! Ibilisi anaweza kutumia hata ndugu yako mliye damu moja
kukuangusha ukimpa nafasi.
Kwa wale walio katika uchumba, angalieni msimpe nafasi Ibilisi kwa kukaa
wawili peke yenu katika maeneo ya siri. Na kwa kutoangalia hili, wengi
wamezini kabla ya siku yao ya harusi. Tunza usafi wa matendo yako, uwe
mwepesi kutofautisha kati ya kupenda na kutamani. Wachumba wanapokuwa
peke yao wawili mara kwa mara, upendo wa Kristo kati yao unapoa na
huwakiana tamaa inayowaongoza kuzini. Usihalalishe ndoa kabla ya siku ya
harusi! Wala usimpe nafasi Ibilisi ya kuwachezea!
Pia, kwako wewe uliyeokoka, mtu wa Mungu, angalia marafiki zako walivyo.
Jihadhari nao. Wengi wameanguka katika zinaa kwa sababu ya marafiki
zao.
(d) MISINGI YA NDOA IHESHIMIWE:
Katika ndoa, walio wengi wameanguka katika zinaa, baada ya kutokea shida
katika uhusiano wa tendo la ndoa.
Kwani maandiko yanasemaje?
“Lakini kwa sababu ya ZINAA kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe,
na kila mwanamke na awe na mume wke mwenyewe, mume ampe mkewe haki yake,
na vivyo hivyo mke na ampe muweze haki yake. Mke hana amri juu ya mwili
wake, bali mumewe; na vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake,
bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpata faragha
kwa kusal; mkajiane tena, shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na
kiasi kwenu.” (1 Wakorontho 7:2-5)
Madhara yanayotokea baada ya kumnyima mke wako au mume wako uhusiano wa
tendo la ndoa ni makubwa. Kwa hiyo, jihadhari usimpe nafasi Ibilisi
katika unyumba wako!
5. ISHI NA ENENDA KWA ROHO:
“Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za
mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana
na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka…..
Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, UASHERATI, uchafu,
ufisadi…… na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo nawaambia mapema
kama nilivyokwisha, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo
hawataurithi ufalme wa Mungu.” (Wagalatia 5:16-21)
“Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho” (Wagalatia 5:25)
“Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili, bali wale
waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni
uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi
kutii. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ikiwa Roho
wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili, bali mwaifuata
roho.” (Warumi 8:5-9).
Ikimbieni Zinaa / 1 / 2 / 3 / 4 /
IKIMBIENI ZINAA
SOMO: IKIMBIENI ZINAA
Wiki ya Nne
UFANYEJE IKIWA UMEANGUKA KATIKA DHAMBI YA ZINAA?
Ni jambo gani linatokea Mkristo anapoanguka katika dhambi ya zinaa? Ni
muhimu ufahamu hili, kabla ya kujua utafanyaje ikiwa umeanguka katika
dhambi ya zinaa.
Mambo matatu makubwa yanatokea mkristo anapoanguka katika zinaa;
(a) Anaukosa Ufalme wa Mungu:
“Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, UASHERATI, Uchafu,
Ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina,
faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo;
katika hayo NAWAAMBIA MAPEMA. Kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba
watu watendao mambo ya jinsi hiyo HAWATAURITHI UFALME WA MUNGU.”
(Wagalatia 5:9-21)
Kumbuka kuwa Mtume Paulo aliandika waraka huu kwa Wagalatia walio
wakristo na siyo kwa Wagalatia ambao siyo wakristo. Waraka unaanza hivi;
“Paulo, Mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali
na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu), na ndugu
wote walio pamoja nami, kwa MAKANISA YA GALATIA” (1:1,2)
Yesu Kristo alisema. “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami
kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. Mimi ni Alfa na Omega mwanzo na
mwisho, wa kwanza na wa mwisho. Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri
kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake. Huko nje
wako mbwa, na wachawi, na WAZINZI, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na
kila mtu apendaye uongo na kuufanya.”(Ufunuo 22:12-15)
Soma pia kitabu cha Waefeso 5:5
(b) Anatengwa na Wakristo wenzake.
Mtume Paulo alipokuwa akiwaandikia wakristo wa Korintho alisema hivi:
“Yakini habari imeenea kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna
isiyokuwako hata katika mataifa….. Mwajivuna, wala hamkusikitika, ili
kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo…..
Naliwaandikia katika waraka wangu, kwamba msichangamane na wazinzi.
Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye
kutamani, au na wanyanganyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo
ingewalazimu kutoka katika dunia. Lakini mambo yalivyo, naliwaandikia
kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye
kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyanganyi;
mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.” (1 Wakorintho 5:1,2-11)
(c) Nchi nzima inaadhibiwa
“Lisikieni neno la Bwana, enyi wana wa Israeli, kwa maana Bwana ana
mateto nao wakaao katika nchi, kwa sababu hapana kweli, wala fadhili,
wala kumjua Mungu katika nchi. Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na
kuvunja ahadi, na kuua na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na damu
hugusana na damu. Kwa ajili hiyo NCHI ITAOMBOLEZA, na kila mtu akaaye
ndani yake ATADHOOFIKA, pamoja na wanyama wa kondeni na ndege wa angani,
naam, samaki wa baharini pia wataondolewa….. Watu wangu wanaangamizwa
kwa kukosa maarifa….. Nao watakula, lakini hawatashiba; watafanya zinaa,
lakini hawataongezeka, kwa sababu wameacha kumwangalia Bwana. Uzinzi na
divai mpya huondoa fahamu za wanadamu” (Hosea 4:1-3; 6,10,11)
Kwa sababu ya uzinzi, gharika iliangamiza watu na vitu vilivyokuwa
katika nchi, alipona Nuhu na watu wachache na viumbe wachache. Kwa
sababu ya zinaa, Sodoma na Gomora iliteketezwa kwa moto, wakapona Lutu
na binti zake wawili.
Na kwa sababu ya zinaa siku hizi nchi zimepigwa kwa ugonjwa wa Ukimwi
(AIDS). Ni kama Nabii Hosea alivyotabiri, NCHI ZINAOMBOLEZA, WATU
WNADHOOFIKA, WANAANGAMIA KWA KUKOSA MAARIFA YA MUNGU, NA WANAPOTELEWA NA
FAHAMU!
Ndiyo maana ni muhimu ufahamu ufanye nini ikiwa umeanguka katika zinaa.
Si mapenzi ya Mungu uangamie, usiurithi ufalme wake, wakristo wakutenge
na kuiangamiza nchi, bali mapenzi yake ni watu wote waifikie toba ya
kweli, waokolewe, waziache njia zao mbaya, na wamgeukie na kumfuata
daima!
Kwa hiyo kama umeanguka katika zinaa, sikiliza ushauri ufuatao:
(i) Usiifiche dhambi:
Najua unaweza kuwaficha wanadamu wasijue umezini,lakini unaweza kwenda
wapi utakakojificha Mungu asikuone? Soma Zaburi ya 139:7-13. Na
imeandikwa:-
“Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha
atapata rehema.” (Mithali 28:13)
Ukifuatilia habari za Mfalme Daudi, utaona ya kuwa kitu alichokifanya
baada ya kuanguka katika zinaa na mke wa mtu, ni kujitahidi kutafuta
namna ya kuifunika hiyo dhambi, lakini alishindwa. Na mwisho wake
aliamua kutafuta mbinu ya kumuua Uria, ambaye mke wake ndiye aliyezini
na Mfalme Daudi. Unaweza ukaona ya kuwa ni kweli kwamba uzinzi huondoa
ufahamu za mtu. Kwa nini Mfalme Daudi aliamua kuua ili alifiche kosa
alilofanya?
Je! Alidhani Mungu naye hajamwona? Mungu aliinua mtu wake, ambaye
alikwenda kwa Mfalme Daudi na kumweleza jinsi Mungu alivyochukizwa na
kitendo hicho. Daudi alipojua dhambi iko wazi mbele za Mungu alitubu!
“Bwana asema hivi, Angalia, nitakuondoshea uovu katika nyumba yako, nami
nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye
atalala na wake zako mbele ya jua hili. Maana wewe ulifanya jambo hili
mbele ya Israeli wote na mbele ya jua. Daudi akamwambia Nathani,
Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa
dhambi yako; hutakufa. LAKINI, KWA KUWA KWA TENDO HILI UMEWAPA ADUI ZA
BWANA NAFASI KUBWA YA KUKUFURU, motto atakayezaliwa kwako hakika yake
atakufa.” (2 Samweli 12:11-14)
Ni kweli kwamba unaweza ukafanya uzinzi kwa siri, Mke wako asijue, au
mume wako asijue, au wazazi wako na ndugu zako wasijue, au waliookoka
wenzako wasijue, Lakini, FAHAMU HAKIKA YA KUWA MUNGU AMEKUONA.
Na mshahara wa dhambi ni mauti, kwa hiyo kama unataka kudumu katika
uzima uliopewa na Kristo, usijaribu kuificha dhambi.
(ii) Tubu, Tengeneza na Usirudie tena.
Ikiwa umeanguka katika dhambi ya uzinzi, njia iliyo wazi ni wewe kutubu
kwa Mungu katika Roho na Kweli,halafu tengeneza (tubu) kwa wale
uliowakosea na usirudie tena; na mwisho songa mbele katika wokovu
aliokupa Bwana.
Kuna mtu mmoja aliniambia nimsaidie katika kumwombea kwa kuwa kuna
wakati alianguka katika zinaa, na baadaye akatubu. Lakini kila wakati
yalikuwa yanamjia mawazo ya kuhukumu ya kuwa alizini na kwa hiyo
anajiona hafai tena hata kuomba wala kuendelea na wokovu. Ingawa alitubu
bado alishitakiwa sana moyoni na kosa alilolifanya. Aliona kama vile
Mungu hajamsamehe.
Inawezekana na wewe ukasumbuliwa na hali ya namna hii. Nafahamu ya kuwa
wanadamu ni wagumu kusamehe na kusahau,hata kama wanajua umekwisha tubu
na kutengeneza.
Lakini nataka nikuambie hivi, usiupime msamaha anaokupa Mungu unapotubu
kwa kuangalia na kusikiliza wanadamu wanasemaje juu yako; bali angalia
neno lake katika biblia linasemaje. Imeandikwa hivi;
“Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na
kama mtu akitenda dhambi anaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye
haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zenu, wala si kwa dhambi zetu
tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote” (1 Yohana 2:1,2)
Tena imeandikwa hivi;
“Tukiziungama dhambi zetu, Yesu ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee
dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” (1 Yohana 1:9)
Tena imeandikwa hivi;
“Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundi
sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundi kama bendera,
zitakuwa kama sufu.” (Isaya 1:8)
Tena imeandikwa hivi;
“Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, Na dhambi zao zitazikumbuka tena”.
(Waebrania 8:12)
Kama ukitubu katika Roho na Kweli, Bwana ameahidi kusamehe na
atakusamehe. Na yeye akisamehe, anafuta kosa lako na kulisahau. Sasa
kama Mungu amesamehe na kusahau, shetani au mwanadamu anapata wapi –
haki ya kukunyoshea kidole cha hukumu? Soma Warumi 8:31-39.
Neno la Mungu ndilo linalokupa uhakika na namna ya kupokea msamaha.
Baada ya kutubu na kutengeneza, simama upya ndani ya Kristo, na songa
mbele kiroho, na katika kumtumikia Bwana. Kwa kuwa “Katika mambo hayo
yote tunashinda na zaidi ya kushinda, kwa yeye (Kristo) aliyetupenda.
(Warumi 8:37)
(iii) Kemea roho ya Uzinzi.
Uzinzi ni roho. Bwana anasema hivi katika kitabu cha Hosea 4:11,12;
“Uzinzi na divai na divai mpya huondoa fahamu za wanadamu. Watu wangu
hutaka shauri kwa gongo lao, na fimbo yao huwahubiri mambo; maana Roho
ya UZINZI imewakosesha, nao wamekwenda kuzini mbali na Mungu wao”.
Baada ya kutubu na kutengeneza, ikiwa bado utaona unasumbuliwa na tamaa
ya kuzini ujue unasumbuliwa na roho ya uzinzi. Kwa hiyo tumia JINA LA
YESU KRISTO ulilopewa, na ikemee roho hiyo nayo itaondoka na kukuacha.
I
Comments
Post a Comment